TUSHIRIKIANE KURUDISHA SOKO LA ALBAMU

MWISHONI mwa wiki Vanessa Mdee alifanya hafla ya kuwasikilizisha mashabiki nyimbo zilizopo kwenye albamu yake ya kwanza, Money Mondays, itakayotoka Januari 15 mwaka huu na kupatikana duniani kote kupitia mtandao wa Boom Play Music.

Hafla hiyo ilifanyika jijini Dar es Salaam  na kuhudhuriwa na mashabiki, wasanii, wadau wa burudani na msanii mwenye asili ya Congo anayeishi Sweden, Mohombi, aliyevuta hisia za wengi kwa kutumbuiza wimbo   wa      Njoo Kwangu uliopo kwenye albamu ya Vanessa.

Hakika hafla hiyo ilitoa mwelekeo wa kule tunakopaswa kuelekea mwaka huu hasa katika upande wa albamu, ambako soko lake lilikwama baada ya kukosekana wasambazaji makini.

Vanessa Mdee amefungua njia na kurudisha matumaini kwa wasanii waliokata tamaa na utamaduni wa kutoa albamu kwa kuwa kupitia yeye tumeona ni namna gani mwanamuziki anaweza kutoa albamu na kupata faida huku akimpa haki ya burudani shabiki.

Ukweli ni kuwa singo moja haikati kiu ya burudani aliyonayo shabiki anayependa kumsikia msanii wake kwenye nyimbo kumi tofauti. Lakini albamu ni kipimo sahihi cha kutambua ukubwa wa msanii husika.

Ndiyo maana Vanessa Mdee kwa kujiamini ameamua kuwasikilizisha mashabiki baadhi ya nyimbo zilizopo kwenye Money Mondays, ili watu wapate picha pana ya ukubwa wake kwenye muziki.

BINGWA tunampongeza Vanessa kwa uthubutu aliouonyesha ambapo bila shaka umewavutia wengi na kuvunja ile mtazamo hasi waliyokuwa nayo wanamuziki wengi juu ya utoaji albamu.

Tunatarajia mwaka 2018 uwe wa wasanii kurudisha nguvu zao kwenye utoaji wa albamu kali zitakazofanya vyema kwenye soko la ndani na nje.

Tunaamini kwamba uzuri mwaka jana kulijitokeza wawekezaji wengi wanaotaka kuboresha usambazaji wa kazi za wasanii hasa albamu.

Hivyo basi, kinachotakiwa ni kuendelea kuunga mkono harakati hizi za kurudisha hadhi ya soko la albamu ili kuwapa moyo wasanii kuendelea kufanya kazi nzuri.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*