googleAds

TUPA KULE Wakali hawa hawatii mguu Afcon 2019

CAIRO, Misri

BAADA ya mechi za kufuzu ambazo zilichezwa kwa mfumo wa makundi, timu 24 zimeshakata tiketi kushiriki fainali za Mataifa Afrika za mwaka huu (Afcon 2019) ambazo zitaanza Juni 29 hadi Julai 19, mwaka huu huko Misri.

Hata hivyo, wakati mashabiki wa kandanda barani Afrika wakisubiri kwa hamu kuanza kwa mashindano hayo, yapo mataifa makubwa yaliyoshindwa kupenya, hivyo kukosekana kwake kutasababisha Afcon 2019 ipoteze baadhi ya mastaa wanaokipiga barani Ulaya.

Pedro Obiang (E. Guinea/West Ham)

Kwa  mashabiki wa Ligi Kuu ya England (EPL), Obiang si jina geni masikioni mwao. Ni kutokana na kazi nzuri ambayo amekuwa akiifanya katika eneo la kiungo la timu hiyo inayoshika nafasi ya 11 katika msimamo wa EPL.

Hata hivyo, kikosi chake cha timu ya taifa ya Equatorial Guinea kilishika nafasi ya tatu katika msimamo wa Kundi A lililokuwa na Senegal, Madagascar na Sudan, hivyo kukosa nafasi Afcon 2019.

Pia, kukosekana kwa Guinea kunamaanisha kuwa Afcon 2019 haitakuwa na beki wa Rayo Vallecano ya La Liga, Luis Meseguer, Carlos Akapo anayecheza nafasi hiyo katika kikosi cha Huesca na kiungo wa Parma, Pepin.

Aubameyang (Gabon/Arsenal)

Pierre Emerick Aubameyang naye hatakuwa Misri. Gabon ya nyota huyo wa Arsenal ilishindwa kufuzu, ikishika nafasi ya tatu Kundi C, ikizidiwa na Mali na Burundi zilizokaa juu yake na kukata tiketi.

Ikishinda mechi mbili na kufungwa mbili kati ya sita, iliungana na Sudan Kusini iliyokamata mkia, hivyo kuikosa michuano ya mwaka huu.

Aidha, si Aubameyang pekee atakayekosekana, pia Gabon kushindwa kufuzu kumeondoka na Mario Lemina wa Southampton, Didier Ndong (Guingamp), Denis Bouanga (Nimes) na Alexander N’Doumbou (Shanghai Shenhua).

Bryan Dabo (Burkina Faso/Fiorentina)

Huyo ni kiungo wa ulinzi mwenye jina kubwa Ligi Kuu ya Italia akiwa na kikosi cha Fiorentina kinachoshika nafasi ya 10 katika msimamo wa ‘Serie A’.

Akitokea Montpellier, aliwahi kutia mguu Ligi Kuu ya England aliposajiliwa na Blackburn Rovers, kabla ya kwenda Saint-Etienne na kisha kuangukia Fiorentina.

Ikiwa Kundi I, Burkina Faso ilishinda mechi tatu na kupoteza mbili, lakini haikuweza kufuzu Afcon 2019 kwani Angola na Mauritania zilishika nafasi ya kwanza na ya pili.

Nyota wengine ni mshambuliaji wa Lyon, Bertrand Traore, kipa anayeidakia Lille, Kouakou Koffi na nyota mwingine kutoka katika timu hiyo ya Ligi Kuu nchini Ufaransa, Amara Ouattara.

Stopila Sunzu (Zambia/Metz)

Miongoni mwa mambo ya kushangaza katika mechi za makundi ni Zambia ‘Chipopolo’ kukosa tiketi ya kwenda Afcon 2019 baada ya kushika mkia Kundi K, ikizibeba Namibia, Msumbiji na Guinea-Bissau.

Kwa kuwa haitakwenda Misri, basi Sunzu, beki wa zamani wa TP Mazembe ambaye sasa anaicheza Metz ya Ligi Daraja la Pili, Patson Daka wa Salzburg, Rainford Kalaba, Kabaso Chongo na Nathan Sinkala wanaocheza TP Mazembe, hawataonekana uwanjani Afcon 2019.

Julio Tavares (Cape Verde/Dijon)   

Kwa kuwa Cape Verde ilimaliza mechi sita za makundi ikiwa mkiani mwa Kundi L, ikizidiwa kete na Uganda na Tanzania zilizochukua nafasi mbili za juu na kwenda zao Afcon 2019, mshambuliaji huyo wa Dijon ya Ufaransa, hatakuwapo huko Misri.

Ukiacha huyo, Cape Verde imewakosesha mashabiki wa soka Afrika mvuto wa nyota kama Nuno Da Costa (Strasbourg), Erin Pinheiro na Kenny Rocha Santos (Saint-Etienne), bila kuwasahau Elber Evora (Feyenoord) na Fernando Varela (PAOK).

Geoffrey Kondogbia (Jamhuri ya Afrika ya Kati/Valencia)

Huyo ni kiungo wa kati wa zamani wa Lens, Sevilla, Monaco na Inter Milan ambaye hatakwenda Misri kwa kuwa timu yake hiyo ya taifa maarufu CAR, haikufuzu baada ya kumaliza mechi sita za makundi ikiwa nafasi ya tatu, nyuma ya Ivory Coast na Guinea zilizofuzu.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*