TUNAHITAJI BURUDANI SIMBA VS YANGA J’MOSI

 

WATANI wa jadi katika soka la Tanzania, Simba na Yanga, wanatarajia kukutana keshokutwa kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam, likiwa ni pambano la mzunguko wa kwanza la Ligi Kuu Tanzania Bara.

Kipute hicho cha kukata na shoka kitakuwa ni miongoni mwa mechi za ligi hiyo zitakazochezwa mwishoni mwa wiki hii kwenye viwanja mbalimbali nchini.

Mechi nyingine ni kati ya Azam FC na Mbeya City kesho kwenye Uwanja wa Azam Complex, wakati Jumapili Kagera Sugar itaikaribisha Ndanda (Kaitaba), Lipuli na Mbao (Samora), Mtibwa Sugar na Singida United (Manungu), Njombe Mji na Stand United (Sabasaba), wakati Majimaji watavaana na Mwadui (Majimaji).

Pamoja na mapambano yote hayo, linalovuta hisia za mashabiki wengi wa soka hapa nchini na kwingineko, ni lile la Simba na Yanga keshokutwa Jumamosi.

Hilo linatokana na ukongwe wa timu hizo, lakini pia utani wa jadi uliopo baina ya klabu hizo zenye mashabiki wengi zaidi nchini na nje ya Tanzania.

Kikubwa katika mchezo huo, mashabiki watakuwa na hamu kuona ni timu gani inamtambia mwenzake, lakini pia wachezaji gani watakaong’ara.

Yote kwa yote, mashabiki watamiminika kwa wingi uwanjani au kuufuatilia kwa karibu mchezo huo kupitia runinga, wakitarajia kupata bonge la burudani kutoka kwa wachezaji wao, kila upande ukijivunia kufanya usajili wa nguvu.

Pamoja na matarajio hayo ya mashabiki, mwisho wa siku BINGWA tunaamini waamuzi ndio watakaoamua watu watoke vipi uwanjani, yaani wawe wameridhika na ushindi au kipigo walichopata au la.

Tunasema hivyo kutokana na uzoefu tulionao kwani mara nyingi timu za Simba na Yanga zinapopambana, waamuzi huwa wanaboronga mno na kuwanyima mashabiki burudani waliyoitarajia.

Wakati mwingine wapo wanaoboronga kutokana na kuchanganyikiwa na ukubwa wa mchezo huo, presha kutoka kwa wachezaji huku wakati mwingine ikidaiwa waamuzi husika kurubuniwa na viongozi wa upande mmoja.

Hivyo basi, tunapolisubiri kwa hamu pambano hilo la watani wa jadi, tuwaombe waamuzi kuchezesha kwa kufuata sheria zote 17 za soka bila kupendelea upande wowote.

Kama kila mmoja wetu anavyofahamu, waamuzi ni sehemu muhimu mno ya mchezo wowote wa soka, inapotokea wanaboronga madhara yake ni makubwa mno kuanzia kwenye matokeo ya mechi husika, usalama wao na mashabiki, lakini pia kwa majaliwa ya soka na wachezaji wetu kwa ujumla.

 

Hivyo ni matumaini yetu waamuzi

watakaochezesha pambano hilo la watani wakiongozwa na Elly Sasii wa Dar es Salaam, watatekeleza majukumu yao ipasavyo kwa kufuata sheria zote 17 za mchezo huo na mwisho wa siku, kupata mshindi atakayestahili kulingana na kile wachezaji wake walichokifanya uwanjani na si vinginevyo.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*