TUENDELEE KUOMBOLEZA AJALI YA KIVUKO CHA MV. NYERERE

JUZI Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo nchini, Dk. Harrison Mwakyembe, alisisitiza mabaraza ya michezo ya Taifa na mashirikisho ya michezo na vyama husika kuendesha shughuli zao kwa kuzingatia siku za maombolezo ya kitaifa, kutokana na maafa ya ajali ya Kivuko cha MV. Nyerere, iliyotokea wiki iliyopita, jijini Mwanza.

Taarifa yake aliyoitoa juzi kupitia kwa Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano serikalini, Lorietha Laulence, ilisema kwamba Waziri Mwakyembe alitoa agizo hilo jijini Mbeya na kuwataka wachezaji na watazamaji wote kusimama kwa dakika moja kabla ya kuanza mchezo ili kuwaombea marehemu wote pamoja na majeruhi wa ajali ya MV. Nyerere.

Katika taarifa hiyo, alitaka kila mchezaji afunge kitambaa cheusi kwenye mkono ikiwa ni ishara ya wanamichezo kuomboleza tukio hilo.

Pia Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), liliungana na Watanzania kwa kutuma salamu za maombolezo kufuatia msiba wa mamia ya Watanzania waliozama katika kivuko hicho.

Salamu zile za TFF ambao ni  wasimamizi wa mchezo wa soka zilikuwa na maana kubwa kwamba, waliofariki katika ajali ile wengine ni wanamichezo.

Ndiyo maana katika mechi za soka zilizochezwa juzi na jana, wachezaji walisimama kimya kwa muda ili kutoa salamu zao za maombolezo kufuatia msiba huo mzito wa taifa.

Tukiwa ni wadau wa michezo, tunaungana na jamii ya Watanzania kuomboleza msiba mkubwa ambao umelikumba Taifa.

Tunasema kwamba, sisi kama BINGWA wateja wetu wa kuwafikishia habari ni kada ya watu wenye furaha ambao katika kipindi hiki wapo katika huzuni na maombolezo makubwa.

BINGWA tunawapa faraja katika kipindi hiki kigumu kwao, lakini tukiwaombea waliotangulia mbele ya haki Mwenyezi Mungu azipokee roho zao na kuziweka mahala pema peponi.

Tunarudia tena kwa kusisitiza kwamba, wadau wa michezo wajione ni sehemu ya tukio hilo na tuendelee kuomboleza. Mungu ibariki Tanzania.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*