googleAds

Tuanze sasa safari Kombe la Dunia 2022

Mwandishi Wetu

DROO ya hatua ya makundi ya mechi za kufuzu fainali za Kombe la Dunia za mwaka 2022 ilichezeshwa siku chache zilizopita, ambapo Tanzania imeangukia Kundi J, pamoja na DRC, Benin na Madagascar.

Kwa Kundi hilo, ni DRC pekee iliyowahi kutia mguu katika fainali hizo za Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa). Hiyo inamaanisha, kama ilivyo Tanzania, Benin na Madagascar nazo zinatafuta nafasi ya kwenda kwa mara ya kwanza.

Hata hivyo, BINGWA tunaamini hiyo si sababu ya kuzibeza Benin na Madagascar. Sote tunambuka walichokifanya Benin katika fainali za Mataifa Afrika mwaka jana (Afcon 2019). Safari yao iliishia robo fainali, wakati Taifa Stars walikwamia hatua ya makundi.

Madagascar nao, licha ya kwamba ilikuwa mara yao ya kwanza kucheza michuano hiyo ya Afcon, nao walifika robo fainali. Kama hiyo haikutosha kushangaza, ilikuwa timu ya kwanza kujihakikishia nafasi ya kwenda kwenye mashindano hayo.

Ukifuatilia viwango vya ubora wa soka vya Fifa, pia unaiona tofauti kubwa kati ya mataifa mawili hayo (Benin na Madagascar) na Tanzania. Benin wako nafasi ya 84, Madagascar wakiwa 91, wakati Tanzania inashika ya 134.

BINGWA hatuna shaka kuwa hayo yanapaswa kuwa angalizo kwa Tanzania kuelekea vita ya kusaka nafasi mbele ya nchi hizo, ukiachialia mbali DRC.

Ni kwa maana hiyo basi, tunaona maandalizi ya mapema yanapaswa kufanywa ili kukabiliana na ugumu wa Kundi J, japo kwa wengine linaweza kubezwa na kuonekana jepesi kwa Tanzania.

Maandalizi ya mapema ni pamoja na kocha Ettiene Ndayiragije kupewa muda mrefu wa kujichimbia kambini na vijana wake. Hilo litapendeza likienda sambamba na kupatiwa mechi za kujipima nguvu, hasa dhidi ya mataifa yanayoshabihiana kiuchezaji na hayo yaliyoko Kundi J.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*