TSHISHIMBI AELEZA MALENGO YAKE YANGA

NA MWAMVITA MTANDA                |          


 

KIUNGO mkabaji wa Yanga, Papy Tshishimbi, ameweka wazi malengo yake katika Ligi Kuu Tanzania Bara msimu ujao na namna atakavyopambana ili kuhakikisha anaisaidia timu yake kunyakua ubingwa.

Kwa sasa kikosi cha Yanga kipo mkoani Morogoro, ambako kimeweka kambi ya maandalizi ya msimu mpya wa Ligi Kuu inayotarajiwa kutimua vumbi Septemba 22, mwaka huu.

Akizungumza na BINGWA jana, Tshishimbi alisema wadau wengi wanafikiri kikosi cha Yanga cha sasa hakina uwezo wa kunyakua ubingwa wa Ligi Kuu msimu ujao, lakini kwa upande wake amejipanga kikamilifu kuhakikisha timu inafanya vizuri.

“Napenda kuiona timu yangu inapata mafanikio, pia malengo yangu makubwa ni kuisaidia timu, hivyo natumaini tutafanya vizuri, maana sasa ni muda wa kazi tu, hatuna muda wa kupoteza,” alisema Tshishimbi.

Aidha, kiungo huyo raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), alisisitiza kwamba, hakuna jambo ambalo litashindikana ikiwa wachezaji na viongozi watakuwa na malengo sawa ya kuisaidia timu, kwani kikubwa kinachohitajika ni ushirikiano.

Hata hivyo, hakusita kupongeza juhudi zinazofanywa na Kocha Mkuu wa kikosi hicho, Mwinyi Zahera, kwani zinasaidia kuiimarisha timu kabla ya kuanza kwa Ligi Kuu.

“Naweza kusema tumepata kocha ambaye anajitoa na kutusaidia, hasa kipindi hiki ambacho tunakabiliwa na kibarua kigumu katika mechi ya hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho ya Afrika dhidi Rayon Sport ya nchini Rwanda,” alisema Tshishimbi .

Katika mechi ya ufunguzi wa msimu mpya wa Ligi Kuu, Yanga itafungua dimba kwa kuvaana na Mtibwa Sugar Septemba 23, mwaka huu, kwenye Uwanja wa Jamhuri, Morogoro.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*