googleAds

Tshabalala alia na Yanga, kisa TP Mazembe

NA WINFRIDA MTOI

BEKI wa Simba, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, amesikitishwa na kitendo cha baadhi ya Watanzania, wakiwamo wanaodaiwa mashabiki wa Yanga, kukosa uzalendo na kuishangilia TP Mazembe walipovaana nayo juzi katika mechi ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Katika mchezo huo uliopigwa kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam, Simba walilazimishwa suluhu huku timu hizo zikitarajiwa kurudiana Jumamosi hii, mjini Lubumbashi, DR Congo.

Akizungumza na BINGWA jana, Tshabalala, alisema anafahamu kuna Watanzania wanashindwa kuziamini timu zao za nyumbani kama zina uwezo wa kufanya vizuri katika michuano mikubwa na kuwatahadharisha kuwa Simba ya msimu huu itawaumbua.

 “Kuna Watanzania hawana uzalendo katika mioyo yao, tunawaangalia tu na sisi tunafanya kazi yetu uwanjani, haiwezekani mtu unashindwa kuamini timu yenu ya nyumbani na unashabikia wageni ila ninawapa salamu waendelee hivyo hivyo,” alisema Tshabalala.

Alisema kitendo cha kutoka sare na TP Mazembe, kiliwafanya wakose furaha kwa sababu walijiandaa kushinda mchezo huo kama walivyofanya katika mechi zilizopita.

“Ujue tulikuwa tumejiandaa kushinda  kwa kuwa mwalimu ametupa mbinu zote  wakati wa mazoezi na tumefanyia kazi maelekezo yake, kutoka sare ni kinyume na matarajio yetu na ndiyo sababu tulitoka uwanjani hatuna furaha,” alisema Tshabalala.

Beki huyo ambaye amekuwa katika kiwango kizuri kwa sasa, alisema wanakwenda kucheza ugenini, hawatakubali kuachia nafasi hiyo kirahisi na wanajua wanachotakiwa kufanya katika mchezo huo.

“Kutoka sare si kama mambo yatakuwa magumu sana kwetu na kushindwa kufanya vizuri, hatuna hofu yoyote tumejipanga hakuna kinachoshindikana, tunachohitaji ni maombi ya Wanasimba katika safari hii,” alisema Tshabalala.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*