TSC ACADEMY WAWAKILISHI WA TANZANIA… KOMBE LA DUNIA LA WATOTO WA MITAANI

 

NA MASYENENE DAMIAN, MWANZA

DUNIA ya soka inasubiria kwa hamu kubwa kuanza kwa michuano ya Kombe la Dunia nchini Urusi, itakayoanza Juni 14, mwaka huu ikishirikisha nchi 32.

Watu wengi wamekuwa wakifuatilia sana     michuano hiyo, lakini kuna mambo mengi hufanyika kabla ya fainali hizo, mojawapo ya hayo ni fainali za Kombe la Dunia kwa Watoto wanaotoka mitaani yaani ‘The Street Child World Cup’ ambayo hufanyika mwezi mmoja kabla ya michuano ya wakubwa.

 

Kombe la Dunia kwa Watoto wa Mitaani

Kwa mara ya kwanza michuano hii inayoshirikisha wachezaji kati  ya miaka 14 na 16 kwa wavulana na wasichana, ilifanyika Machi, 2010 mjini Durban, nchini Afrika Kusini, ikishirikisha mataifa saba, ikiwamo Ufilipino, Nicaragua, Brazil, Ukraine, India na Tanzania, ambapo timu husika inakuwa na wachezaji Tisa wakiwamo watatu wasichana.

Katika michuano hiyo, India ilitwaa ubingwa baada ya kuifunga Tanzania iliyowakilishwa na TSC Academy ya Mwanza, bao 1-0, huku Ufilipino wakiwa washindi wa tatu na Ukraine kuwa timu yenye nidhamu.

Mashindano hayo yalifanyika kwa mara ya pili mwaka 2014 nchini, Brazil, ambapo safari hii nchi za Afrika ziliongezeka zikiwamo Misri, Sierre Leone, Kenya, Mauritius na Burundi na kufanya washiriki wafikie 16.

Awamu hiyo Tanzania ilitwaa ubingwa katika fainali iliyozikutanisha timu za Afrika, ambapo TSC Academy (wawakilishi wa Tanzania) waliibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Burundi, huku Pakistan ikiwa mshindi wa tatu.

Hivyo mwaka huu michuano hiyo ya watoto yenye kauli mbiu ya ‘ The Future Depends On You’, yatafanyika nchini Urusi kwa mara ya tatu, ambapo hushirikisha michezo, matamasha ya sanaa na kongamano la haki za watoto wakilenga kubadilisha mtazamo hasi na kasumba juu ya watoto wa mitaani.

 

TSC Academy

Kituo cha TSC Academy (Tanzania Street Children), kilianzishwa mwaka 2009 na     kipo wilayani Ilemela, Mkoa wa Mwanza, kikisaidiwa na wadau mbalimbali, ambapo kinajumuisha watoto walio chini ya umri wa miaka 13 na 17 kwa wasichana na 12, 14 na 17 kwa wavulana na kwa sasa kituo hicho kina jumla ya watoto 130 wanaocheza soka.

Kilishiriki kwa mara ya kwanza michuano ya Kombe la Dunia mwaka 2010, nchini Afrika Kusini, kikipeleka timu ya wavulana chini ya miaka 16 na kuambulia nafasi ya pili baada ya kufungwa na India bao 1-0 kwenye fainali.

Kilishiriki tena mwaka 2014 nchini Brazil na kufanikiwa kuwa mabingwa baada ya kuilaza Burundi mabao 3-0 kwenye fainali, ambapo kituo hicho kinashiriki tena safari hii nchini Urusi kikipeleka timu ya wasichana chini ya miaka 17 ya wachezaji tisa katika michuano hiyo inayotarajia kutimua vumbi Mei 10, mwaka huu.

Moja ya mafanikio ya TSC Academy ni kuwa na timu inayocheza Ligi Daraja la Tatu Mkoa wa Mwanza na wasichana iliyoshiriki ligi ya wanawake mkoa na mwaka jana na kushika nafasi ya pili nyuma ya mabingwa Alliance Girls, pia imefanikiwa kutoa wachezaji mbalimbali akiwamo Kelvin Sospeter, Emmanuel Amos aliyekuwa golikipa bora wa Kombe la Dunia mwaka 2014 na Abdulkarim Segeja anayekipiga Mbao FC.

Timu hiyo iliagwa jana (Jumamosi) na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella, ambapo aliikabidhi bendera ya Taifa akiwataka wafanye vizuri na waliwakilishe taifa.

Kocha Mkuu wa Kituo cha TSC Academy, Daniel Yangwe, alisema matarajio yao makubwa ni kufanya vizuri kama wanavyofanya miaka yote na kurudi na kombe nyumbani.

“Safari hii tumeamua tupeleke timu ya wasichana, matarajio yetu ni kufanya vizuri kama tunavyofanya miaka yote, nchi zitakazoshiriki ni 24 za wasichana na wavulana na tunatarajia kuondoka Mwanza Mei 8, mwaka huu kuelekea Dar es Salaam ambako tutaondoka Mei 9, kuelekea Urusi kwa    sababu mashindano yanaanza Mei 10, mwaka huu,” alisema.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*