TRY AGAIN AWAGAWA SIMBA

NA ZAITUNI KIBWANA                  |              


 

KITENDO cha Kaimu Rais wa Simba, Salim Abdallah ‘Try Again’, kutochukua fomu kuelekea uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika Novemba 30, mwaka huu, kimewagawa wadau wa klabu hiyo.

Try Again alianza kukaimu nafasi hiyo kuanzia Julai 2, 2017 baada ya kuteuliwa na Kamati ya Utendaji kuchukua nafasi ya Rais, Evans Aveva ambaye anatuhumiwa na makosa mbalimbali, ikiwemo ya utakatishaji fedha.

Kiongozi huyo kipenzi cha mashabiki na wanachama wa Simba, amegoma kuchukua fomu kwa kudai akigombea atatafsiriwa kuwa alifanya mabadiliko ya uendeshaji wa klabu kutoka mfumo wa wanachama kwenda wa hisa kujitengenezea mazingira ya kuongoza.

Wakizungumza na BINGWA kwa nyakati tofauti, wapo wadau wa Simba waliompongeza kiongozi wao huyo, huku wengine wakimpinga.

Katibu wa Tawi la Simba la Tandika Koma, Mohammed Mchewa, amempongeza Try Again kwa kutumia demokrasia ya kuwapisha wengine tofauti na watu walivyotarajia.

“Tunamshukuru, huyu ndiye kiongozi, kuna watu wanataka wakae madarakani weee hadi wachokwe. Tunaomba wale watakaopata nafasi nao wafanye mazuri kama yaliyofanywa na kiongozi huyu (Try Again),” alisema.

Kwa upande wake, mchezaji wa zamani wa timu hiyo, Fikiri Magoso, alisema hajafurahishwa na uamuzi huo kwa kuwa Try Again ni kiongozi aliyekuwa anahitajika Simba.

“Try Again ni kiongozi mzuri, nimesikitika kwa kweli, anastahili kuwa Simba, anafaa kuendelea kutuongoza, ametupa mafanikio makubwa katika kipindi kifupi alichokaimu,” alisema.

Naye mchezaji na kocha wa zamani wa timu hiyo, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’, alipata kigugumizi na kusema kuwa hayupo tayari kuzungumzia chochote kinachohusu uchaguzi.

Katika uchaguzi huo, wajumbe sita wataingia kwenye Bodi ya Wakurugenzi inayosimamiwa na mwekezaji wa klabu hiyo, Mohammed Dewji ‘Mo’.

Wagombea waliochukua fomu wameanza kurudisha na mwisho ni Jumamosi tayari kwa usaili unaotarajiwa kufanyika mapema wiki ijayo.

Wagombea ambao wamechukua fomu kuwania nafasi ya urais Simba ni mchezaji wa zamani wa timu hiyo na timu ya Taifa, Taifa Stars, Mtemi Ramadhani na Swed Mkwabi.

Kwa upande wa wajumbe waliochukua fomu ni Hussein Mlinga, Iddi Kajuna, Ally Kaduguda, Mohammed Wandi, Seleman Said, Abdallah Mgomba, Christopher Mwansasu, Alferd Elia, Mwina Kaduguda, Ally Suru, Said Tulliy, Juma Pinto, Hamis Mkoma, Abubakari Zebo, Omary Mazola, Patrick Rweyemamu na Seleman Omary Seleman.

Kwa upande wa wanawake, waliojitosa kuwania ujumbe ni Asha Baraka na Yasmin Badar Soudy.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*