TRBA YAWAONYA WAAMUZI WASIOFUATA SHERIA

NA OSCAR ASSENGA, TANGA

CHAMA cha Mpira wa Kikapu Mkoa wa Tanga (TRBA), kimetishia kuwapokonya leseni waamuzi watakaopindisha sheria na kutoa upendeleo kwa baadhi ya timu katika michuano ya Ligi ya Mkoa itakayoanza Aprili 20, mwaka huu.

Ligi hiyo itachezwa kwa mfumo wa nyumbani na ugenini na itashirikisha timu tano ambazo zitashindana ili kumpata bingwa wa mkoa ambaye baadaye atashiriki mashindano ya ngazi ya kanda.

Akizungumza jana Katibu Msaidizi wa chama hicho, Patrick Semindu, alisema msimu huu wamedhamiria kurudisha heshima ya michuano hiyo kwa kuweka mazingira ambayo yataondoa upendeleo kwa waamuzi watakaochezesha.

Alizitaja timu zitakazoshiriki mashindano hayo kuwa ni Tanga United, Bandari, Deepsea, Korogwe Hits na Shule ya Sekondari Galanosi na viwanja ambavyo vitatumika ni Mkwakwani, Bandari na Galanosi.

“Mara nyingi waamuzi wamekuwa wakipindisha sheria na kanuni za ligi kwa makusudi hali inayochangia kuharibu ladha za mashindano, hivyo nawaambia kwenye ligi ya mkoa tutakuwa wakali kwa yeyote atakayebainika na ikiwezekana watanyang’anywa leseni,” alisema.

Hata hivyo, alieleza kuwa watafanya hivyo kwa lengo la kuhakikisha wanaondoa rushwa kwenye mashindano hususani ya mkoa ili kuweka usawa ili kumpata bingwa halali.

“Ligi hii itakuwa inachezwa kila mwishoni mwa wiki ili kutoa fursa kwa klabu kujiandaa kikamilifu kwa mashindano, pia kuwapa wachezaji nafasi ya kufanya shughuli nyingine katikati ya wiki,” alisema Mguto.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*