TP MAZEMBE 4-1 SIMBA…Lubumbashi ni mwanzo wa safari mpya ya Simba Afrika

NA AYOUB HINJO

ILIKUWA siku nyingine kwa mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba, kucheza mchezo wao wa pili wa robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Katika mchezo huo, zilikutana timu mbili zenye malengo tofauti, wenyeji walihitaji kusonga mbele ili kuweka hai matumaini ya kutwaa taji hilo kubwa, huku Simba walihitaji kuandika historia mpya tu.

Ndio, Simba wameandika historia ingawa katika mchezo huo uliopigwa kwenye Uwanja wa TP Mazembe, waliondoka vichwa chini kwa kukubali kichapo cha mabao 4-1.

Pamoja na hayo yote kutokea, inabidi lichukuliwe kama somo kwa timu hiyo kutoka Tanzania ambayo imeandika historia mpya Afrika msimu huu.

Tunaweza kusema Simba waliifanya Tanzania kujulikana zaidi katika ramani ya soka la Afrika, ilikuwa rahisi kuitafuta nchi hii kwenye ‘Google’ au kuisaka kwenye ramani ya dunia.

Kwa namna moja au nyingine, Simba wanatakiwa kuwekeza nguvu katika michezo ya Ligi Kuu Tanzania Bara ili kuweza kurudi kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao.

Simba wanaonekana kuwa bora kila kukicha, hakuna kingine zaidi ya michezo ya kimataifa ambayo wamekuwa wakicheza hivi karibuni.

Walicheza dhidi ya Mbabane Swallows ya Swaziland, Nkana FC ya Zambia kabla ya kutinga makundi ambako walipangiwa Al Ahly ya Misri, AS Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na JS Saoura ya Algeria.

Hata hivyo, wametolewa katika hatua ya robo fainali ya michuano hiyo na TP Mazembe, ni mafanikio makubwa kwa Simba hivi karibuni.

Uzoefu walioupata kwenye michezo hiyo ni chachu ya timu hiyo kufanya vizuri kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara, wanajifunza mambo mengi ambayo yana faida ndani ya kikosi hicho.

Makosa ambayo walikuwa wakiyafanya mara kwa mara yanaonekana kupungua kila siku, wanakuwa bora kila jua linapochomoza hapa nchini.

Ili uwe bora lazima ushindane na aliyekuzidi, kwa hatua waliyofikia Simba inabidi wakomae kweli kuweza kufika kwenye lengo lao kuu hata kama isipofanikiwa watakuwa wamejifunza mambo mengi ya kujenga.

Kama uliwahi kung’atwa na nyoka, hata jani likikugusa lazima utashtuka, kazi kubwa ya Simba ni kuhakikisha wanafanikiwa kurudi kwa mara nyingine kwenye makundi msimu ujao.

Hiyo maana yake wanahitajika kushinda taji la Ligi Kuu Tanzania Bara kwa mara nyingine ili kufika walipofika, hilo likishindikana itakuwa ni kama hasara kwa Simba ambao tunaweza kuwahesabu walipiga hatua tatu mbele na kurudi nane nyuma.

Ubora wa Simba ndani ya uwanja usiishie kwenye michezo ya Ligi Kuu Tanzania Bara tu, kufanya vizuri Afrika inabidi uwe na uhakika wa kushiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa au Shirikisho kila msimu, huku ukiwa na uhakika wa kufika hatua za mbali zaidi.

Mchezo wa soka umetawaliwa na uwekezaji wa wachezaji wenye uwezo mkubwa, kama unahitaji kuwa sehemu ya timu kubwa za Afrika na ikiwezekana duniani.

Licha ya kuwa na wachezaji wenye uwezo na ubora mkubwa, bado mbinu za makocha zina nafasi kubwa ya kuamua matokeo, ukitoa uwezo binafsi wa wachezaji.

Ubora na uwezo wa Simba utazidi kukua kama watakuwa na nafasi ya kushiriki mara kwa mara michuano hiyo ya Afrika wala isiwe kutoka na kuingia kama zamani.

Ikumbukwe mara ya mwisho Simba walitinga hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 2003, zaidi ya miaka 10 wanapata nafasi nyingine ya kuingia hatua hiyo.

Hilo halitakiwi kutokea tena kama wanataka kufika mbali zaidi, tayari wametolewa katika Kombe la Shirikisho la Azam ambalo linatoa nafasi kwa bingwa kushiriki michuano ya Kombe la Shirikisho la Afrika.

Njia pekee ya Simba kushiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika imebaki Ligi Kuu Tanzania Bara ambako wapo nafasi ya tatu katika msimamo, nyuma ya Yanga na Azam ambao wamecheza michezo mingi zaidi.

Kama wakifanikiwa kurudi kwa mara nyingine kwenye michezo ya kimataifa, itakuwa ni mafanikio makubwa zaidi lakini endapo kama watafanikiwa kutwaa taji la Ligi Kuu Tanzania Bara.

Ukubwa wa Simba ndani ya Tanzania unatakiwa kupimwa Afrika pia, hakuna njia nyingine zaidi ya kushindana dhidi ya Al Ahly, TP Mazembe, Esperance Tunis, Mamelodi Sundowns, Wydad Casablanca na wengine wengi.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*