TOTTENHAM V MAN UNITED: REKODI ZA NYUMBANI, UGENINI ZITAMALIZA UBISHI WEMBLEY

LONDON, England

NI kesho katika Uwanja wa Wembley ambako Tottenham watakuwa wenyeji wa Manchester United ya kocha Jose Mourinho.

Huo utakuwa ni mchezo wa 25 kwa kila timu tangu kuanza kwa msimu huu wa Ligi Kuu England (EPL).

Spurs watashuka dimbani wakiwa na kumbukumbu ya kupata sare katika mchezo wa ligi uliopita dhidi ya Southampton.

Kikosi hicho cha kocha Mauricio Pochettino, kinashika nafasi ya tano kwenye msimamo wa ligi, kikiwa kimeshajikusanyia pointi 45.

Kwa upande wa Man United, wao wataingia kuzisaka pointi tatu wakiwa na nguvu ya ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Yeovil Town katika mtanange wa Kombe la FA.

Mourinho na vijana wake wako nafasi ya pili nyuma ya Man City, wakiwa na pointi 53 walizozivuna katika mechi 24.

Kuelekea mtanange wa kesho usiku pale Wembley, hizi ni dondoo zitakazoufanya kuwa kivutio kikubwa kwa mashabiki wa soka ulimwenguni kote.

Vita inaanzia hapa

Mtanange wa kesho ni muhimu kwa timu zote na hilo ndilo litakaloufanya uwe mkali na unaovutia kuutazama.

Spurs wenye pointi 45, watahitaji ushindi ili kuingia ‘top four’, nafasi ambayo kwa sasa inashikiliwa na Liverpool.

Lakini pia, Man United watakapopoteza kesho, basi watakuwa wamepunguziwa kasi ya kuwakimbiza Man City walio kileleni mwa msimamo kwa tofauti ya pointi 12.

Mbali na hilo, watakuwa wameiweka rehani nafasi yao ya pili ambayo inanyemelewa na Chelsea.

Rekodi za nyumbani, ugenini

Licha ya kwamba Spurs watakuwa nyumbani, wasitarajie mteremko kwa Man United. Watambue kuwa Mashetani Wekundu hao wameshacheza mechi 12 za ugenini msimu huu na wameshinda saba na kutoa sare tatu.

Lakini pia, Man United nao wasichukulie poa kwani Spurs wamekuwa hatari zaidi wanapokuwa nyumbani katika Uwanja wa Wembley.

Katika mechi 12 walizocheza mbele ya mashabiki wao msimu huu, wameshinda saba, wakatoa sare nne, hivyo wamefungwa moja pekee.

Katika mechi tano zilizopita kwa kila timu hakuna iliyopoteza, Spurs wameshinda tatu na kutoa sare mbili, Man United wao wamechekelea ushindi mara mbili na kutoa sare tatu.

Mvua ya mabao

Hapa kutakuwa na balaa kubwa hiyo kesho, ikizingatiwa kuwa timu zote zina safu kali za ushambuliaji.

Tangu kuanza kwa msimu huu, Spurs wameshafunga mabao 47, huku wakiruhusu nyavu zao kutikiswa mara 22.

Man United nao wako moto katika ushambuliaji kwani wameshaziona nyavu za wapinzani mara 49 na kuruhusu mabao 16.

Zimekutana mara ngapi, ikawaje?

Ukiacha mchezo wa kesho, timu hizo zimeshakutana mara 157 na ni Man United ndiyo inayoongoza kwa kuibuka na ushindi (81).

Huku Sours wakishinda mara 36, mechi 40 zilizobaki zilimalizika kwa matokeo ya sare.

Katika mitanange mitano iliyopita kati ya timu hizo, Spurs wameshinda miwili na Man United wakacheka mitatu.

Na hata ule wa mwisho ambao ulichezwa Oktoba 28, mwaka jana, katika Uwanja wa Old Trafford unaoingiza mashabiki 74,994, ni Man United ndio walioibuka na ushindi wa bao 1-0.

Vikosi

‘First eleven’ ya Spurs inatarajiwa kuwa na Hugo Lloris, Aurier, Sanchez, Vertonghen, Davies, Dier, Dembele, Eriksen, Alli, Son na Kane.

Kwa upande wa Man United, kikosi cha kwanza cha Mourinho kitakuwa na De Gea, Valencia, Lindelof, Jones, Shaw, Matic, Pogba, Herrera, Sanchez, Rashford na Lingard.

Macho kwa Sanchez, Kane

Kuna uwezekano mkubwa wa Alexis Sanchez kucheza mechi yake ya kwanza ya Ligi Kuu England akiwa na ‘uzi’ wa Man United.

Hata hivyo, wengi watataka kuona kama ataweza kuwafunga Spurs ambao aliwatungua wakati alipoiwezesha Arsenal kupata ushindi wa mabao 2-0 katika mchezo uliochezwa Novemba.

Huku Sanchez akitolewa macho, pia wengi watakuwa wakimtazama Harry Kane. Si tu kwa sababu ndiye kinara wa mabao akiwa amepasia nyavu mara 21, bali rekodi yake ya kumliza Mourinho.

Katika mechi nne zilizopita dhidi ya timu za kocha huyo, Kane amechangia upatikanaji wa mabao manne, akifunga matatu na kutoa ‘asisti’ moja.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*