googleAds

TIZI LA SIMBA KAMA ULAYA

NA MAREGES NYAMAKA

MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba, waliendelea na tizi la nguvu kujianda na mchezo ulio mbele yao Ijumaa hii watakapowakaribisha Mtibwa Sugar katika Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.

Katika mazoezi hayo yaliyofanyika viwanja vya Gymkana, kilichovutia zaidi kabla ya tizi lenyewe ilikuwa ni aina ya usafiri wa wachezaji wa Simba ambayo kila mmoja aliwasili nayo kama ambavyo tumekuwa tukishuhudia huko Ulaya.

Wanandinga hao ambao wanatokea majumbani mwao waliwasili kila mmoja akiwa na gari lake binafsi, huku mengi yakiwa ya bei mbaya zaidi hususan kwa wachezaji wenye majina makubwa akiwamo nahodha, John Bocco.

Bocco ambaye aliwasili wa mwisho kabisa alikuwa akiendesha mwenyewe mkoko wake aina ya Harrier ya kisasa yenye thamini ya Sh. milioni 35, huku mchezaji mwenzake mwandamizi, Erasto Nyoni, yeye akiwa na Mark X ambayo thamani yake ni Sh. milioni 25.

Nyota mwingine mwenye mkoko kama wa Nyoni yaani Mark x ni beki wa kati, Kennedy Juma, pamoja na kipenzi cha wengi, Ibrahim Ajib, akiendesha Crown kama ilivyo kwa Gadiel Michael na Hassan Dilunga ambazo bila Sh. milioni 25  utabaki kuingalia tu yadi.

Kipa Beno Kakolanya, anakula kiyoyozi ndani ya Mark 11 ya kisasa yenye thamani ya Sh. milioni 15, beki mwingine wa kati, Yusuf Mlipili hapandi tena boda bado kama zamani hivi sasa anaendesha Toyota Swift inayogharimu Sh. milioni tisa.

Lakini pia nahodha msaidizi, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, aliwasili na Raum huku Muzamiru Yassin yeye mdogo mdogo akatinga na IST.

Baada ya mazoezi hayo kumalizika, kila mmoja aliingia kwenye ndinga lake na kurejea nyumbani huku kocha, Patrick Aussems, akibainisha namna alivyokiandaa kikosi chake kuwatungua Mtibwa Sugar.

“Mtibwa Sugar ni timu nzuri na wazoefu wa ligi, ni mchezo mzuri kwa timu zote mbili, lakini sisi tunachoangalia ni alama tatu,” alisema.

Licha ya asilimia kubwa ya wachezaji hao wanaotetea ubingwa wa Bara kuwa na magari yao, lakini bado gari maalumu kwa ajili ya wachezaji lilikuwa limeegesha pembeni likisubiri wale watakaoamua kulitumia.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*