Tiboroha alishadhamiria kuinusuru Yanga kabla ya mkwamo

NA Mwandishi Wetu

HATA kabla ya kukutana na kuzungumza naye ana kwa ana, nilimsikia Dk. Jonas Tiboroha, akizungumza katika vyombo vya habari juu ya maono na mikakati yake kuhusu klabu yake ya Yanga aliyokuwa akiiongoza wakati huo kama Katibu Mkuu.

Alikuwa na mtazamo mpana zaidi wa kuijenga Yanga inayoweza kujitegemea bila ufadhili wa mtu mmoja, aliamini katika ukubwa wa Yanga yenye mtaji mzuri wa mashabiki wa kweli wenye mapenzi ya dhati na klabu yao. Ni kwa bahati mbaya sana kwamba mikakati na mipango mizuri ya Dk. Tiboroha ilimezwa kabisa na hali ya ufadhili mzito uliowekwa na aliyekuwa Mwenyekiti wa klabu hiyo, bilionea Yusuf Manji.

Hakika haikuwa rahisi kwa kiongozi yeyote anayeingia Yanga kuweka mkakati mzuri wa kiuchumi wa kuisadia Yanga ukaonekana wakati wa kipindi cha Manji.

 Wakati huo, wanachama na wapenzi wengi wa Yanga waliamini kwamba kila kitu kingefanyika, kwani mwenyekiti wao ni bilionea na wengi hawakuwa na mawazo ya kesho ya Yanga itakuwaje baada ya kuondoka bilionea.

Hali ya kutowaza Yanga bila bilionea Manji, ndiyo iliyosababisha Wanayanga kutoifikiria kesho ya klabu yao na ndiyo maana kila aliyejitokeza kutaka kumpa changamoto bilionea huyo kwa namna yoyote alionekana adui, tena adui hasa.

Bilionea alipigiwa magoti, alibembelezwa, wapo wa baadhi ya Wanayanga ambao upeo wao uliishia kumwona bilionea pekee mbele ya mafanikio ya Yanga.

 Walisahau kabisa kwamba bilionea kama mtu alikuwa kiongozi na siku moja angeondoka kama ambavyo aliondoka na kuiacha Yanga kama klabu ikiendelea na maisha yake.

Dk. Tiboroha aliliona tatizo la Yanga kuwa na mfumo tegemezi hasa kwa mtu mmoja. Akiwa kama Mtendaji Mkuu wa klabu alianza kufanya michakato ya kuisaidia Yanga kupata mapato zaidi ya mfumo wa mtu mmoja. Aliamini hilo lingeweza kujenga Yanga imara yenye nguvu zaidi katika soka la kisasa.

Katika mazungumzo naye mwanzoni mwa mwaka 2006, muda mfupi kabla ya kuondoka Yanga  alizungumzia juu ya mikakati imara anayoijenga kuhakikisha Yanga inakuwa na mfumo madhubuti wa udhamini ambao utaihakikishia mapato mengine nje ya kumtegemea aliyekuwa mwenyekiti.

Ni bahati mbaya baadhi ya Wanayanga hawakumwelewa, walikuwa wakinufaika na uwepo wa Mwenyekiti Manji, wakamchukia pengine kwa kutoelewa kwao au kwa maslahi yao binafsi kwa aliyekuwa Mwenyekiti wao. 

Dk. Tiboroha akaondoka Yanga, maneno yalikuwa mengi lakini hakujibu, hata nilipomtafuta tena alinitaka tuzungumzie maendelo ya mpira na si yeye na klabu yake ya Yanga.  

“Njoo tuzungumzie maendeleo ya soka, sio mimi na Yanga, sitaki kuiumiza Yanga kwa kuizungumzia dhidi ya mtu mwingine yeyote maana nitakuwa najiumiza mwenyewe,” alinijibu wakati nikiweka miadi ya kutaka kuonana naye.

Sasa Dk. Tiboroha anataka kurejea Yanga kama kiongozi mwenye ridhaa ya wanachama, anataka nafasi ya juu ambayo itamwezesha kuwa na mamlaka ya kuwaamulia Wanayanga kwa manufaa ya klabu. Akiwa na mtazamo mpana zaidi wa kuifanya klabu hiyo kwenda katika mfumo bora zaidi, Dk. Tiboroha anataka kuijenga Yanga yenye uchumi imara usiotegemezi kwa watu bali kwa mifumo yake yenyewe. 

Pengine kama angepewa nafasi na uongozi uliomwajiri angeweza kujenga mfumo ambao leo hii ungeisaidia Yanga isifike hapa ilipo. Aliliona tatizo hili likija na akaliwekea mkakati lakini hata kabla hajautekeleza akaondolewa. 

Yanga sasa inahitaji viongozi wenye mikakati na si wenye maneno mengi, soka la sasa linahitaji mikakati imara na madhubuti na si porojo za kuwahadaa wanachama. Soka linahitaji kuongozwa na wasomi waliosomea masuala ya uongozi wa michezo na si ngojera. 

Yanga inahitaji viongozi wanowiwa na si wanaohemkwa, viongozi wanoongozwa na maoni na si mihemko, viongozi watakaojenga na kupanga mikakati ya kuifikisha kwenye uwekekezaji mkubwa unaoonekana na hali ya soka la kisasa duniani kote.

Wanachama wa Yanga wanayo nafasi nzuri sasa kufanya maamuzi yaliyobora kwa klabu yao. Wapo wagombea wengi, wengine walishaiongoza Yanga huko nyuma kwa nafasi za juu lakini walishindwa kuikwamua. Yanga inahitaji watu wenye mitazamo na mawazo mapya. 

Timu ya wananchi inahitaji mwananchi wa kweli kuivusha na kuiondoa katika hali hii ya sasa ya kutembeza bakuli.

Endelea kusoma BINGWA UPATE MAKALA ZA WAGOMBEA WENGINE YANGA


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*