THIBAUT COURTOIS AKIOKOA BAO MOJA ANALIPWA MIL 200/-

LONDON, England

KAMA huna taarifa nikwambie tu kwamba usidhani mabeki wa Chelsea wakipotea basi nyavu zao zimetikisika.

Nyuma yao kuna jembe Thibaut Courtois, ni mmoja kati ya walinda mlango mahiri kuwahi kutokea Ligi Kuu England.

Tangu kuanza kwa msimu huu, Mbelgiji huyo ameokoa mashuti 17 na ameiongoza Chelsea kukwea kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu England.

Kuna taarifa zisizo na shaka kuwa kipa huyo raia wa Ubelgiji huweka mfukoni pauni 100,000 (zaidi ya Sh mil 200) kila anapookoa shuti linalotinga wavuni.

Courtois hajafungwa katika mechi sita za ligi zilizopita na kwa mara ya mwisho nyavu zake zilitikiswa Septemba katika mchezo dhidi ya Liverpool.

Katika mchezo wa Jumapili ya wiki iliyopita, kama si Courtois kuokoa bao la wazi la Alvaro Negredo katika dakika ya 78, huenda Chelsea wangeukosa ushindi mwembamba wa bao 1-0.

Michezo mitatu iliyopita Courtois ameokoa mashuti mawili yaliyokuwa yakitinga wavuni.

Wachambuzi wengi wa soka wanaamini kipa huyo wa zamani wa Atletico Madrid ndiye nguzo imara ya safu yake ya ulinzi.

Wanaamini kuwa Courtois amekuwa sehemu muhimu ya mfumo wa 3-4-3 ambao hutumiwa na kocha Muitalia Antonio Conte.

Kwa upande wake, baada ya kuwachapa Middlesbrough, Courtois aliwaambia waandishi wa habari kuwa anaupenda mfumo huo kwa kuwa umekuwa ukizisumbua timu pinzani.

“Kwa kweli umeleta mabadiliko makubwa na ni ngumu kwa timu nyingine kuuzoea.

Mchezo ambao ulikuwa mgumu kwa Courtois ni dhidi ya Manchester United, kwani alilazimika kuokoa michomo mitano iliyokuwa ikielekea kwenye nyavu zake.

Mechi dhidi ya Everton, Leicester City na Burnley zilikuwa nyepesi mno kwani hakufanya kazi yoyote.

Mpaka sasa, kipa huyo mwenye umri wa miaka 24 ndiye anayeongoza kwa kusimama langoni muda mwingi bila kuruhusu nyavu zake kutikiswa.

Hata hivyo, Chelsea wanatakiwa kukaza buti ili kuifikia rekodi ya Manchester United ambao walicheza mechi 14 bila kufungwa na hiyo ilikuwa katika msimu wa 2008-09.

Hata anapokuwa langoni kwenye kikosi cha timu yake ya taifa ya Ubelgiji, bado Courtois amekuwa habari nyingine.

Itakumbukwa kuwa katika michezo mitatu iliyopita akiwa na timu hiyo, mlinda mlango huyo amefungwa bao moja pekee.

Lakini mtihani mwingine kwa Courtois ni Jumamosi ya wiki hii ambapo Chelsea watavaana na mahasimu wao wa jijini London, Tottenham.

Swali pekee lililobaki vichwani mwa mashabiki wengi wa soka ni je, ataendelea kuvuna pauni 100,000 kwa kuzuia mashuti ya straika Harry Kane?


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*