googleAds

TFF KAZENI MACHO FDL KUMEANZA KUHARIBIKA

LIGI Daraja la Kwanza imeshika kasi na sasa ipo katika mzunguko wa pili. Ligi hiyo inayochezwa katika makundi matatu ndiyo itatoa timu tatu zitakazopanda kucheza Ligi Kuu soka Tanzania Bara msimu ujao.

Mshindi wa kila kundi kwenye ligi hiyo inayoshirikisha timu 24 zilizogawanywa kwenye makundi ya timu nane kila kindi, inapata nafasi ya kucheza Ligi Kuu. Hali ya kutaka kupanda ligi kuu imekuwa ikichochea ushindani kwa baadhi ya timu za ligi hiyo ushindani ambao umeripotiwa kwenda mbali zaidi ya ule wa uwanjani.

Wakati ligi hiyo ikiingia katika mzunguko wa pili, masuala kadhaa yameanza kujitokeza huku malalamiko yakiongezeka kwa baadhi ya timu kwamba zimepangwa kupanda daraja msimu huu hivyo zimekuwa zikifanyiwa upendeleo wa hali ya juu katika mechi zao.

Kutokana na hali hiyo, mechi kadhaa zimekumbwa na utata jambo ambalo limesababisha pia kuibuka kwa vurumai baina ya wachezaji na waamuzi hasa kutokana na wachezaji kutokubaliana na maamuzi yanayotolewa dhidi ya timu zao.

BINGWA tunalitaka Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuongeza umakini kwenye usimamizi wa ligi hii ili kuhakikisha kwamba washindi wanapatikana kihalali na timu zinazopanda daraja zinapanda kutokana na jasho la uwanjani na si kwa mipango kama ambavyo inaonekana sasa.

Ni vyema TFF wakawa wakali katika hili ikiwa ni pamoja na kuwaonya maofisa wake ambao wamekuwa kwa namna moja au nyingine wakijihusisha na vitendo vya upangaji wa matokeo ili kuzisaidia baadhi ya timu kupata kile kinachohitaji kama ambavyo ilishuhudiwa msimu uliopita.

Tunayo kumbukumbu mbaya ya msimu uliopita juu ya suala la upangaji matokeo, hivyo tusingependa kuona suala hilo linajitokeza tena msimu huu hasa kutokana na ukweli kwamba masuala hayo yanaishia kutuletea Ligi Kuu timu ambazo hazina ubora na mwisho wa yote huishia kushuka daraja tena msimu unaofuata.

Aidha, BINGWA tunaamini timu zinazopanda daraja kwa kubebwabebwa ndizo hizo ambazo huja na kuiharibu ligi kuu kwa sababu msukumo wa kubebwa hutegemea tena wanapofika ligi kuu na wanapoikosa hujikuta timu hizo zikiwa watumwa na viongozi wao kuwa walalamikaji kila siku wanapofungwa.

Ni muhimu TFF ikaongeza umakini katika kipindi hiki ambapo figisufigisu zimeanza kushamiri kwenye michuano ya ligi hiyo ambapo baadhi ya sehemu yameripotiwa matukio ya ushirikina na kwingine vimeripotiwa vitendo visivyo vya kiungwana vyote vikiashiria timu fulani kutaka ushindi wa kupangwa wa nje ya uwanja jambo ambalo halina tija kwenye soka letu kwa sasa.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*