TETEMA… Madrid watumia mwezi mmoja kuitikisa La Liga

MADRID, Hispania

KIKOSI cha Real Madrid kimekamilisha muda wa mwezi mmoja wa kupindua vita ya kuwania ubingwa wa La Liga msimu huu, kutokana na ushindi wao wa mabao 3-1 dhidi ya wapinzani wao wa jadi, Atletico.

Hata hivyo, ushindi huo ulizua maswali kutokana na maamuzi ya utata ya VAR, yaliyowalazimu Atletico kuhoji suala hilo kwa ‘kuposti’ picha kadhaa zinazoonesha matukio tofauti wanayodai hayakuwa sawa kwa upande wao.

Kimchezo, Madrid walikuwa bora zaidi uwanjani na kocha wa Atletico, Diego Simeone, alisisitiza baada ya kumalizika kwa mechi hiyo kuwa VAR haikuwa sababu ya wao kupoteza mchezo huo.

Simeone alisema wachezaji wake walizidiwa na hasira kutokana na maamuzi ya utata yaliyokuwa yakitolewa, ukiwemo wa kuwapa Madrid penalti iliyotokana na Vinicius Jr kuanguka baada ya kuguswa mguuni na beki, Jose Gimenez.

Hata hivyo, Atletico waliposti picha iliyoonesha kuwa tukio hilo lilitokea nje ya boksi la penalti.

Aidha, Atletico walilalamikia maamuzi mengine ya kukataa bao la Alvaro Morata kwa madai aliotea, lakini picha zilionesha straika huyo alikuwa sawa na Ramos katika mstari wa kuotea pamoja na kunyimwa penalti baada ya Morata kuangushwa na Casemiro ndani ya 18.

Ukiachana na malalamiko hayo ya Atletico, ukweli ni kwamba Madrid imetumia muda mfupi sana kubadilisha mwenendo wao uwanjani, kwa kuuanza mwaka 2019 na matokeo ya sare ya mabao 2-2 dhidi ya Villarreal.

Matokeo hayo yalionekana kama ndio mwanzo wa anguko kubwa la Madrid, lakini baadaye kikafuatia kichapo cha mabao 2-0 kutoka kwa Real Sociedad na kujikuta ikiachwa na vinara, Barcelona, kwa tofauti ya pointi 10.

Lakini, tangu walivyopoteza mbele ya Sociedad, Madrid imeimarika na kupata matokeo mazuri yaliyowasogeza hadi kwenye nafasi ya pili katika msimamo wa La Liga, huku wakiwa na nafasi ya kutinga fainali Copa del Rey.

Madrid iliilazimisha sare ya bao 1-1 Barcelona, kwenye nusu fainali ya kwanza ya michuano hiyo, mechi iliyochezwa kwenye dimba la Camp Nou.

Kuanzia Januari mwaka huu mpaka kufikia sasa, Madrid imeshinda jumla ya mechi nane, kichapo kimoja na sare moja (dhidi ya Barca).

Baadhi ya wachezaji walioipaisha Madrid katika muda huo ni beki chipukizi wa kushoto, Sergio Reguilon, wakongwe Toni Kroos, Luka Modric na Karim Benzema.

Aidha, kocha wa timu hiyo, Santiago Solari, amekuwa na msaada mkubwa kwa kuwapa morali vijana wa timu hiyo kuanzia Reguilon, Marcos Llorente na winga, Vinicius.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*