TEAM ‘FITNA’ YA SIMBA YATUA MTWARA

NA ZAINAB IDDY

VINARA wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Simba wanatarajia kuondoka keo kwenda Mtwara kuikabili Ndanda FC, lakini uongozi wa timu hiyo umetanguliza timu ya watu kwa ajili ya kuandaa mikakati na kuhakikisha timu yao haifanyiwi vitendo vya hujuma.

Wekundu wa Msimbazi wanatarajia kucheza na Ndanda katika mchezo wa marudiano wa Ligi Kuu Tanzania Bara, utakaochezwa Jumapili kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona, huku watu wao wa fitina wakiwa wametangulia kuanzia jana.

Miongoni mwa watu ambao wanasifika kwa kuwa na fitina kali ni wale waliowatanguliza kwenda Misri kwa ajili ya kucheza na Zamalek ya nchini humo na kufanikiwa kusonga mbele katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika katika msimu wa 2003.

Katika mchezo huo wa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa, Simba walihitaji sare baada ya kupata ushindi wa bao 1-0 nyumbani, lakini Zamaleck walipata ushindi kama huo kwao na baadaye kuamuliwa kwa mikwaju ya penalti ili kumpata mshindi ambaye angeingia hatua ya robo fainali, ambapo Simba walipenya kwa penalti 4-3.

Simba wanaongoza katika msimamo wa ligi hiyo kutokana na pointi 35, ikiwa ni tofauti ya pointi mbili kwa Yanga wanaowafuatia, wanahitaji kushinda dhidi ya Ndanda ili waweze kuendelea kujisafishia njia ya kutwaa ubingwa msimu huu.

Kabla ya kikosi hicho kuondoka jijini Dar es Salaam, kilikuwa kikifanya mazoezi ya mwisho kwa siku mbili mfululizo kwenye Uwanja wa Boko Veterani kujiandaa na mchezo huo ambao ni muhimu kwao kushinda.

Lakini taarifa zilizopatikana ndani ya klabu hiyo zilieleza kwamba ili kuhakikisha wanashinda wametanguliza baadhi ya vigogo ambao waliwahi kuiongoza klabu hiyo.

Mtoa habari wetu alisema vigogo hao wametangulia ili kuweka mazingira sawa, kwani watasubiri wachezaji wao wakiwa mafichoni.

“Timu itaondoka kesho (leo), lakini kuna viongozi wenye nafasi kubwa ndani ya klabu (majina tunayo) wametangulia kwani si unajua lazima tukaandae mazingira mazuri yatakayotupa ushindi katika mechi yetu.”

Katika hatua nyingine, kocha wa timu hiyo, Joseph Omog, ameonekana kukamilisha maandalizi ya mchezo huo.

Mazoezi ya juzi yaliyofanyika kwa takribani saa tatu, Omog alitumia muda mwingi kuwafua washambuliaji na mabeki, lakini akiwataka kupiga pasi fupi kwa haraka ili kuwakabili ilivyo wapinzani wao.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*