googleAds

TATIZO NI TOFAUTI YA VIPAUMBELE VYA KOCHA NA VIONGOZI TFF

NA LEONARD MANG’OHA

SIKU kadhaa zilizopita Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) lilisitisha mkataba wa aliyekuwa kocha mkuu wa timu ya Taifa, Taifa Stars, Charles Boniface Mkwassa “Master.”

Kusitishwa kwa mkataba wa Mkwassa kulionekana kuibua hisia na maswali kadhaa miongoni mwa wapenda soka wengi nchini, wengine wakihusisha uamuzi huo na misimamo ya kocha huyo ambayo amekuwa akiionyesha akiwa kocha wa Stars.

Kabla ya Mkwasa tutakumbuka kuwa Stars iliwahi kunolewa na Mbrazil Marcio Maximo kati ya 2006 na 2010, ambapo Stars ilifanikiwa kutinga katika fainali za michuano cha CHAN inayoshirikisha wachezaji wanaocheza soka la ndani ya Afrika.

Wakati huu ndipo tulishuhudia Stars ikizitoa jasho timu kama Burkina Faso kwa kuifunga nyumbani na ugenini ikazitetemesha timu kama Cameroon, Senegal, Zambia na Ivory Cost.

Kipindi hiki ndipo walau Tanzania iliweza kujisogeza katika nafasi za 90 katika viwango vya ubora wa soka duniani na kuanza kuitangaza nchi katika medani za soka ambazo ziliyashawishi mataifa kama Brazil kuja kucheza mechi za kirafiki.

Silaha kuu ya Maximo ilikuwa ni imani yake juu ya vijana baada ya kuwakusanya wachezaji wachanga kama Jerryson Tegete, Kigi Makasi, Amir Maftah na Mrisho Ngassa, ambao walipingwa na wengi baada ya kusafiri mara kadhaa pasi na kucheza mechi lakini baadaye walionyesha uwezo mkubwa hasa kwa Tegete aliyekuwa mfungaji bora kwa kipindi chote ambacho Maximo aliinoa Stars.

Pamoja na jitihada zake alizozifanya hatimaye mkataba wake ulifikia ukingoni na jukumu la Stars likatua kwa  Mdenimark, Jan Poulsen, ambaye alianza kwa kunyakuwa ubingwa wa Chalenji Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) akitumia kikosi kilichoandaliwa kwa muda mrefu na Maximo, hapo akapewa sifa nyingi na wasiolifahamu soka na waliozoea kuendesha mambo kwa njia za mkato baada ya hapo mambo yakaanza kumwendea mrama akaishia kutimuliwa.

Nafasi yake ilitwaliwa na Mdenmark mwenzake Kim Paulsen ambaye pia aliweza kufanya vizuri na akikumbukwa zaidi kwa kuilaza Morocco kwa mabao 3-1.

Kim alikuwa na mkakati mzuri, lakini wakati TFF ikiwa kwenye mihangaiko cha uchaguzi mkuu wa viongozi wa TFF, walishindwa kuweka akili zao kwa timu ya Taifa hivyo kujikuta akifanya vibaya lakini uongozi ulioingia haukuona kama anafaa hivyo ukamtimua.

Hapa waswahili wakaja na hoja ya timu ya Taifa akabidhiwe mzawa kwa kile walichodai kuwa wageni hawana uzalendo, hapa macho ya waongoza jahazi la soka nchini yakaangalia Uholanzi na kuibuka na Mart Nooij, ambaye hata hivyo matokeo yake hayakuwa rafiki kabisa katika mioyo ya Watanzania naye akatupiwa virago.

Hoja ya kocha mzalendo iliendelea na hapo sasa pengine kwa aibu viongozi wa TFF wakatua Jangwani na kumwibua Mkwassa aliyekuwa kocha msaidizi wa Yanga, akapewa mikoba.

Sasa Mkwassa ameondoka na timu ipo mikononi mwa Salum Mayanga, tayari tunaingia kwenye michuano ya Afcon 2019 miezi michache ijayo, je, tunaingia tukiwa na Mayanga ambaye alikuwa msaidizi wa Nooij na tukafeli?

Tanzania kama mchi kisoka tatizo letu kubwa si makocha wazawa au wazungu, tatizo kubwa lipo kwenye mfumo wetu wa uendeshaji wa soka, kuanzia ngazi ya klabu hadi kwenye Taifa kwa maana ya TFF.

Angalia timu gani ya ligi kuu yenye akademi ya kukuza vipaji kwa vijana ili kupata wachezaji kwa matumizi ya baadaye na hata kwa masuala ya kibiashara? Bila shaka ni Azam pekee, hapa utabaini mfumo wa soka letu ndio kikwazo kikuu cha maendeleo ya mchezo huo.

Kalimangonga Ongalla ni Kocha Mkuu wa Majimaji ya Songea, anasema makocha wamekuwa hawapewi muda wa kutosha kukaa na timu ya Taifa na licha ya makocha kuwa na mipango mizuri, lakini mipango ya makocha haiendani na mipango ya viongozi wa soka ndiyo tatizo kubwa.

“Tatizo ni kwamba, watu wengi wanaangalia Azam, Simba na Yanga wakiamini kuwa wachezaji wazuri wako katika timu hizo tu, hata mimi mwanzo wakati najiunga na Azam niliamini kuwa Azam kuna mipango mizuri na wachezaji wazuri kuliko hizi timu ndogo.

“Nilipokuja Majimaji nikagundua hata huku kuna wachezaji wazuri na wenye vipaji na ndio hawa wanaotoka hizi timu zinazoitwa ndogo na kujiunga na Azam, Yanga na Simba,” anasema Kally.

Anasema kuboronga kwa Stars si tatizo la makocha wala wachezaji na suluhisho pekee kujenga mfumo mzuri utakaosaidia kukuza vipaji vya vijana kuanzia umri mdogo ili kuwaweka katika hali ya ushindani na kujiamini.

“Lakini pia mfumo ambao hautaingiliana na siasa za uongozi  wa soka, tatizo kubwa lililopo ni kwamba, viongozi wetu wa soka wana programu zao, vipaumbele vyao na mipango yao, ambayo nina uhakika kabisa huwa inatofautiana na vipaumbele, programu na mipango ya kocha na ndiyo maana tunakwama,” anasema.

Anasema kuna wadau wanadhani kwamba makocha inabidi wazunguke nchi nzima kuangalia vipaji, lakini wanazungukaje nchi nzima, wanaanzia wapi? Kuna academy gani za kuangalia huko mikoani?

“Ulifanyika mpango wa maboresho ulikwama kwa sababu ulikuwa ni mkakati wa kisiasa kwenye soka, sasa hatuwezi kutoka hapo kama mipango na programu za makocha wa taifa Stars zinatofautiana na mipango na programu za viongozi wa TFF,” anasema.

Kally amekwenda mbali zaidi na kuwashutumu hadi waandishi wa habari  kwa kudai kwamba wanaandika kishabiki na kuangalia kuuza magazeti, lakini inapaswa waandishi waandike kusaidia kukuza soka.

Naye mchambuzi wa soka na mchezaji wa zamani, Ally Mayay, anaitaja Serikali kama mdau mkubwa anayepaswa kusimamia soka na kulifanya lilete mafanikio.

“Serikali ikiingiza mkono na kuweka mazingira mazuri itasaidia kuwavuta wadau wengine kuwekeza kwenye soka la vijana, sasa hivi wengi hawataki kuwekeza kwa sababu hakuna faida,” alisema Mayay.

Anasema ikiwa Serikali itawezesha kuwapo mfumo mzuri Taifa litapata wachezaji bora na makocha wazuri wala hakutakuwa na shida ya kubadili makocha kila mara.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*