Tanzania yashinda nafasi ya tatu kuogelea Afrika

NA MWANDISHI WETU

TIMU  ya taifa ya mchezo wa kuogelea ya Tanzania (The Tanzanite) imeshinda Kombe la Shaba katika michuano ya Kanda ya Tatu Afrika iliyomalizika, Nairobi, Kenaya Jumapili  iliyopita.

Tanzania iliyowakilishwa na waogeleaji  25 imemaliza nafasi ya tatu katika michuano iliyoshirikisha nchi tisa za Afrika kwa kukusanya pointi 2, 044.50.

Wenyeji  Kenya ilimaliza nafasi ya kwanza kwa kupata pointi 2, 447.50 na kufuatiwa na Uganda iliyopata pointi  2, 392.

Mbali ya kushinda nafasi hiyo, waogeleaji watatu wa Tanzania, Sydney Hardeman, Romeo Mihaly na Sylvia Caloiaro walishinda vikombe kwa kushika nafasi ya kwanza kwa waogeleaji.

Sydney alipata pointi 130  kwa waogeleaji wenye miaka kati ya 11-12, wakati Romeo alikusanya pointi 118 katika umri huo na Sylvia alipata pointi 126.

Kwa matokeo hayo, waogeleaji wa kike wa Tanzania waling’ara zaidi kwa kumaliza nafasi ya pili kutokana na pointi 1,083 huku Kenya wakishika nafasi ya kwanza kwa kupata pointi 1,180  na Uganda wakimaliza nafasi ya tatu kwa pointi 851.

Kwa upande wa wanaume, Tanzania ilipata pointi 865.5  na kushika nafasi ya tatu nyuma ya Kenya iliyomaliza ya pili kwa kupata pointi 1, 143.50 na Uganda iliyokuwa ya kwanza kwa pointi  1, 421.

 Matokeo yanaonyesha kuwa Afrika Kusini imeshika nafasi ya nne kwa kupata pointi 1, 540 wakati nafasi ya tano imekwenda kwa Zambia kwa kupata pointi  1,386 na Burundi ya sita kwa kupata pointi 866.

Waliokuwa mabingwa watetezi, Sudan imeshindwa kufukuta baada ya kushika nafasi ya saba kwa kupata pointi 812 huku Djibouti ikipata pointi 105 na  Malawi ikipata pointi  88.

Timu ya Tanzania iliundwa na waoegeleaji Maria Bachmann, Sylvia Caloiaro, Kayla Temba, Sydney Hardeman, Linnet Laiser, Sophia Latiff, Sarah Shariff, Avalon Fischer, Nawal Shebe, Roos Nevelsteen, Eunike Mathayo na Lissa Stanley.

Wengine ni Mischa Ngoashani,  Augustino Lucas, Romeo Mihaly, Delhem Rashid, Terry Tarimo, Aaron Akwenda, Singko Steiner, Ethan Alimanya, Sil Kleinveld, Ezra Miller,  Augustino Lucas,  Ashraf Moez, Nathan Kagoro, na Peter Itatiro.

 @@@@


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*