TANZANIA WENYEJI MBIO ZA NYIKA AFRIKA 2020

NA GLORY MLAY


SHIRIKISHO la Riadha Afrika (CAAA), limeliomba Shirikisho la Riadha la Tanzania (RT) kuwa mwenyeji wa Mashindano ya Mbio za Nyika Afrika 2020.

Rais wa CAAA, Hamad Kalkaba, aliwasiliana na Rais wa RT, Anthony Mtaka, kumpa ombi hilo huku akiwa pamoja na Rais wa wa Dunia wa Riadha (IAAF), Sebastian Coe.

Akizungumza na BINGWA jana, Katibu Mkuu wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), Wilhelm Gidabuday, alisema wamepokea ombi hilo na hivi sasa wanasubiri ratiba kamili kutoka CAAA.

“Itakuwa ni mara ya kwanza Tanzania kuandaa mashindano makubwa kama haya, IAAF na CAAA wanayo imani kubwa na Tanzania kutokana na maandalizi ambayo tumewahi kufanya ya mashindano ya EAAR.

“Bado hatujaamua mashindano hayo yafanyike wapi, lakini ili kutangaza utalii wetu bila shaka yatafanyikia mikoa ya Arusha au Kilimanjaro sababu ya uwepo wa mahitaji muhimu kama vile Uwanja wa Ndege wa KIA, hoteli za kutosha, mbuga za wanyama na vivutio vingine,” alisema.

Mashindano hayo huwa yanatokana na hali ya hewa, hivyo huenda yakafanyika kuanzia mwenzi wa Machi na Aprili.

Ikumbukwe Tanzania ilimaliza nafasi ya 6 katika mashindano ya dunia yaliyofanyika Kampala mwaka jana, mashindano yajayo ya Nyika ya Dunia yanatarajiwa kufanyika Machi 30, 2019 nchini Denmark.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*