TAMASHA LA WASAFI LIMEBEBA MATUMAINI MAPYA

NA MAREGES NYAMAKA

HATIMAYE kampuni ya Wasafi Media ambayo Mkurugenzi wake ni mwanamuziki, Naseeb Abdul ‘Diamond Platnumz’, imeweka wazi mpango wa kukata kiu ya mashabiki wa muziki nchini Tanzania na Kenya kupitia Tamasha la Wasafi (Wasafi Festival).

Mapema jana uongozi wa Wasafi Media walikutana na vyombo mbalimbali vya habari jijini Dar es Salaam, lengo likiwa ni kuanika utaratibu mzima wa tamasha hilo lenye sura ya kuleta mapinduzi katika tasnia ya muziki nchini.

Miongoni mwa mikoa ambayo tamasha hili lililojipambanua vyema kufanya kazi na wasanii wote wanaofanya vizuri hata wale ambao hawapo katika lebo ya WCB, ni Mtwara, Novemba 24 mwaka huu katika Uwanja wa Nang’wanda Sijaona.

Novemba 30, mwaka huu wakazi wa Iringa watashuhudia burudani kutoka kwa wasanii watakaopata nafasi ya kutumbuiza katika Tamasha la Wasafi, ambalo pia litagusa maisha ya wakazi wa mkoa huo.

Mkoa mwingine ambao Tamasha la Wasafi litapita ni Morogoro, Desemba 2 mwaka huu huku mikoa mingine ikiendelea kutembelewa na kadiri muda unavyozidi kwenda bila kusahau Mombasa na Nairobi, Kenya.

Kama tunavyofahamu licha ya uwepo wa matamasha kadhaa ya muziki nchini ambayo yanaendelea, Diamond anaamini kwa namna walivyojipanga Wasafi Festival litakuwa ni tamasha la tofauti kutokana na mikakati yao huku kauli mbiu yao ikiwa ni Mchezo, usiuchezee kabisa wewee!!.

Diamond Platnumz aliweka bayana watakavyofanya matukio ya kurudisha fadhila kwa jamii siku chache kabla ya tamasha hilo kufanyika kwenye mkoa husika kama vile kutoa madaftari, sare, madawati na kukarabati miundombinu kwenye shule zenye mazingira magumu.

Pia, Wasafi Festival linakwenda kuwagusa wanawake wanaojishughulisha wakiwa na mawazo chanya, wanatazamwa kwa jicho la kipekee ikiwamo kuwawezesha shilingi 200,000 za mitaji.

Hali kadhalika kundi la vijana halijaachwa, kwani Diamond Platnumz na jopo lake watakutana na vijana na kuzungumza nao kwa kina juu ya namna ya kutumia mitandao ya kijamii kwa faida wakishirikiana na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).

Hata hivyo, anaweka wazi kuwa kutakuwa na vitu vingi atakavyofanya kwa jamii kulingana na eneo husika wanapowasili, huku nyuma yake akiwepo mwanamitindo maarufu, Flaviana Matata, atakayeshughulika na kuwanyanyua wanamitindo wa mkoani.

Wasafi Festival pia litawahusisha mastaa wa muziki kutoka nje ya Tanzania kama Nigeria na Marekani, ambao ni marafiki wa lebo ya WCB ili kunogesha zaidi na kuwaonyesho kuwa Bongo tunaweza kufanya matamasha makubwa kama wao.

Suala jingine ni kufanya kazi vizuri na waandishi wa habari, kwani tumeshuhudia waandaaji wa matamasha mengi wakiwatumia wasanii pale wanapotangaza ishu zao lakini huwatelekeza wanapofanikisha adha yao.

Tamasha hilo limejipambanua kujali maslahi ya wasanii kwa kuwalipa vizuri jambo ambalo huwa tunaona wasanii wengi wakilipwa fedha kidogo licha ya kutumia fedha nyingi kuandaa maonyesho yao.

Jambo zuri zaidi ni vile ambavyo Diamond Platnumz kutangaza nia yake ya kumwona ‘hasimu’ wake, Ali Kiba, akishiriki katika tamasha hilo ili kuua ile dhana ya kuwa na bifu lisilo na faida.

Hali kadhalika matumaini ya mashabiki, wadau na wasanii ni kuona wale wasanii wakali ambao wana mashabiki wengi lakini kutokana na sababu za hapa na pale, hawapati nafasi ya kutumbuiza wanalitumia jukwaa hilo kuburudisha.

Mfano ni Godfrey Tumaini ‘Dudu Baya anayevuma hivi sasa kwa a.k.a yake ya Konki Konki Master, amekuwa haonekani kwenye majukwaa mengi licha ya kuwa nyuma yake ana mashabiki, kupitia tamasha hilo Diamond ametamani rapa huyu atumbuize.

 


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*