TAKUKURU YAANZA KUTOA USHAHIDI KESI YA RUSHWA VIGOGO TFF

NA KULWA MZEE

OFISA Uchunguzi kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini  (Takukuru), Sosthenes Kibwengo,  amedai vigogo wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF),  waliomba rushwa ya Sh milioni 25 ili wagawane na  vigogo wenzao.

Mgawo ulikuwa wa makundi matatu, kundi la kwanza Sekretarieti ya TFF, Sh milioni 10, Uhamiaji Sh milioni tano na Kamati ya Sheria na Hadhi ya wachezaji  Sh milioni 10.

Kibwengo alidai jana alipokuwa akitoa ushahidi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shahidi, akiongozwa na Wakili wa Serikali, Leonard Swai.

Vigogo hao wa TFF wanaotuhumiwa kuomba rushwa kwa viongozi wa Klabu ya Geita ni Rais msaidizi wa TFF, Juma Matandika na kaimu mkurugenzi wa mashindano wa shirikisho hilo, Martin Chacha.

Shahidi alidai Februari 4 mwaka huu, Salum Kulunge na Constantine Morandi ambao ni viongozi kutoka Chama cha Soka Mkoa wa Geita na Klabu ya Geita, walifika TFF kwa ajili ya kusikiliza rufaa ya mchezaji Mohammed Jingu wa timu ya Polisi Tabora, ambaye aliwekewa pingamizi kuwa si raia wa Tanzania,  hivyo usajili wake ulikuwa batili.

“Viongozi hao walifuatilia kwa sababu Geita ililingana pointi na Polisi Tabora katika kundi C, uamuzi ungekuwa mbaya kwa Jingu, wao wangefaidika kwa timu yao kupanda daraja.

“Februari 4 walikutana na washtakiwa ambao waliomba rushwa ya Sh milioni 25 ili iwe kishawishi cha kutoa uamuzi kwa faida yao, viongozi hao wa Geita walirekodi mazungumzo yote.

“Sh milioni 25 zilizoombwa zilikuwa zigawanywe katika makundi matatu, kundi la kwanza Sekretarieti ya TFF Sh milioni 10, Uhamiaji Sh milioni tano na Kamati ya Sheria na Hadhi ya Wachezaji Sh milioni 10,” alidai.

Ofisa huyo alidai walipofanya uchunguzi walipeleka tape kwa Katibu Mkuu wa TFF kwa ajili ya kuisikiliza kutambua sauti na katibu huyo alizitambua sauti za washtakiwa.

Upande wa jamhuri katika kesi hiyo walidai wana mashahidi 10 na vielezo ikiwemo hiyo tape.

Upande wa utetezi ulidai una mashahidi wanne, mahakama iliahirisha kesi hadi Desemba 5 mwaka huu.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, washtakiwa wanakabiliwa na kosa moja la kuomba rushwa kinyume cha sheria ya kuzuia rushwa.

Wanadaiwa Februari 4 mwaka huu, makao makuu ya TFF wakiwa waajiriwa wa TFF waliomba rushwa ya Sh milioni 25 kutoka kwa Salum Kulunge na Constantine Morandi kama kishawishi kwa TFF na Idara ya Uhamiaji Tanzania kutoa uamuzi dhidi ya Klabu ya Mpira wa Miguu Polisi Tabora ili kuisadia Klabu ya Geita kupanda katika Ligi Kuu Tanzania.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*