TAJIRI WA MASIKINI -31-

Ilipoishia

“Kuna sheria moja iko ndani ya bustani ambayo wote waliopewa nafasi ya kufanya majaribio waliivunja sijui wewe,” aliongea kiasi cha kuniogopesha sana.

“Sheria gani dada?” niliuliza kwa woga wa hali ya juu.

“Ulipofika eneo la mwisho kabisa bila shaka ulimuona msichana?” aliniuliza.

 “Ndio nimemuona.”

 “Umemsemesha?”

 “Hapana.”

 “Una hakika?”

 “Ndio hata kuniona hajaniona.”

 “Kwanini hukumsemesha?”

 “Kwa sababu kazi yangu ilikuwa ni kuihudumia bustani na sio kingine bosi wangu.”

Niliposema hivyo, alitabasamu kwa dharau kisha akachukua kalamu na kuandika jambo kwenye karatasi yake. Baada ya kumaliza alichukua kadi moja na kunikabidhi, kadi hiyo ilikuwa na alama ya tajiri Alexender Rugoa, niliipokea huku nikitetemeka mwili.

 “Kadi hiyo itakuwezesha kufika tena hapa kwa urahisi, kote kwenye ulinzi utapita na kuonesha hiyo. Kesho kutwa rudi hapa ili ujue kama umepata kazi au la, sawa?” aliongea dada huyo mzuri kwa dharau ile ile ya mbali.

SASA ENDELEA

Hakika moyo wangu ulifarijika sana, nilijikuta nashuka chini kumpigia magoti dada huyo. Ingawa sikuwa nimepata kazi lakini kitendo cha kuambiwa kuwa nirudi kesho nilijiona ni mwenye bahati sana.

“Inuka uende,” aliongea kwa majivuno kidogo.

“Asante sana dada Mungu akubariki kwa wema wako huo.”

“Unanishukuru sana unadhani kazi utapata? Labda leo na kesho ukamuomba sana Mungu ili aniongoze, kwa sababu kumbuka kuwa mimi ni Mhai na wewe ni Mpache kukupa kazi ni nguvu za Mungu sio zangu,” aliongea tena kwa majivuno ya mbali.

Niliiweka vizuri ile kadi niliyopewa nikiificha vizuri sana kwenye mfuko wangu wa suruali. Nilitoka kwenye kile chumba kwa nidhamu zote na unyenyekevu wa hali ya juu kama vile nilikuwa natoka mbele ya kiti cha mfalme.

Nilibeba mfuko wangu wenye vifaa vya bustani na kuanza kupiga hatua kuelekea lango kuu. Mara kadhaa nilikuwa nikigeuka nyuma kuliangalia jengo la tajiri Alexender Rugoa lililokuwa kama makazi ya malkia wa Uingereza Elizabeth. Nilipotembea umbali mrefu kidogo, nilifika lango kuu na kukutana na yule mfungua lango, mtu aliyekuwa na dharau iliyopitiliza.

Nilipomkaribia alinitazama sana akianzia chini hadi juu utadhani ndio mara yake ya kwanza kuniona. Inaonyesha hakuamini kama nilikuwa nimepewa majaribio, hakika alinistaajabu.

“Kijana fukara inaonyesha una Mungu wako wa ziada tofauti na yule ninayemwabudu mimi,” aliongea kwa dharau.

Mimi sikumjibu nilibaki kumtazama tu nikisubiri anifungulie mlango ili nitokomee zangu, alipoona sifungui mdomo wangu, alielekea langoni  na kunifungulia, nikiwa natoka aliniambia kwa kicheko cha dharau.

“Nadhani hutafika tena hapa wasalimie kwenu Adorra.”

Niliondoka kwenye lango hilo na kusogea mbele kidogo, ambapo niliwakuta wale askari walinzi, niliwapa salamu ya heshima zaidi nikitoa shukrani zangu kwao, walifurahi sana kuona nimewaheshimu kiasi kile.  Nilitoka hapo na kuendelea na safari nikipita njia hiyo ya tajiri Alexender Rugoa, taratibu nikiliacha eneo zima la himaya yake.

Nilivuka  njia yake na kuingia barabara nyingine ya mtaa huo wa matajiri, baadhi ya wasichana warembo waliokuwa wakitembea kwa miguu ambao ni wakazi wa maeneo hayo walikuwa wakinicheka sana huku wengine wakipigwa na butwaa kubwa kuniona masikini kama mimi nikiwa nimeruhusiwa kuingia mtaani kwao.

**********

Baadaye kabisa ikiwa ni saa 12 jioni, nilikuwa natoka kabisa mtaa huo wa matajiri ulioitwa  Movan Mero. Nilianza kushika njia ya kuelekea mtaa wa Kampont, mtaa aliokuwa akiishi rafiki na ndugu yangu Rahimu, mtu niliyemheshimu sana. Kulikuwa na umbali mrefu sana kutokea Movan Mero hadi Kampont, nilitembea sana baada ya kuchoka sana, ilinilazimu kupanda usafiri wa umma maana giza lilikuwa tayari limekwishaivamia nchi.

Nilipanda basi dogo hadi karibu na njia inayoelekea Kampont ambapo nilishuka na kuanza kutembea kwa miguu nikielekea nyumbani kwa Rahimu. Hata hivyo, nilikuwa nahofu sana kuelekea kwake  kwa sababu ya mkewe alikuwa hapendi kabisa kuniona.

Nilitaka kulala nje lakini kwa kuwa nilikuwa natamani sana kumsimulia  Rahimu yale niliyojionea kwa tajiri wa Afrika, Alexender Kai Rugoa, ilinilazimu kuonana naye usiku huo huo. Tokea natoka ndani ya lile hekalu, picha ya yule msichana niliyemwona kama malaika, ndani ya bustani ya maajabu, haikufutika kabisa usoni mwangu kila baada ya dakika kadhaa nilimkumbuka sana.

Nilifika kwa Rahimu saa 2:30 usiku, niligonga mlango mara mbili, baada ya dakika moja alikuja mkewe kufungua mlango, aliponiona alibaki kunishangaa sana huku akiwa na ndita nyingi za hasira.

“Unataka nini usiku huu?” aliniuliza.

“Habari za jioni shemeji.”

“Sio nzuri niambie umefuata nini usiku huu.”

“Samahani kwa usumbufu shemeji sijui Rahimu nimemkuta?”

“Hayupo.”

“Hajarudi bado kutoka mihangaikoni?”

“Nimekwambia hayupo, naomba uondoke.”

Akiwa ananiambia hayo, nilisikia sauti ya Rahimu akimuuliza kutokea ndani.

“Mama Jafaa kuna mgeni hapo mlangoni?”

“Hakuna mtu mume wangu.”

Alifunga mlango na kuniacha nimesimama nje, niliamua kugeuka na kuanza kuondoka, bahati nzuri Rahimu alinichungulia dirishani na kuniona, haraka aliniita.

“Vanuell!”

Niligeuka na kumtazama, nilisikia akimgombeza mke wake kwa kitendo alichokifanya, alimtolea maneno makali sana, baadaye alikuja kufungua mlango na kusema.

“Njoo rafiki yangu samahani sana.”

Nilimsogelea kwa unyonge wangu na kufika mlangoni.

“Habari yako ndugu yangu samahani sana nadhani tabia ya mke wangu unamjua, nisamehe mimi,” aliongea akiwa amenishika bega.

“Usijali besti yangu ni kosa langu sikutakiwa kuja usiku huu nyumbani kwako.”

“Hapana Rahimu hapa ni kwako muda wowote njoo hata usiku mnene wa manane wewe njoo tu.”

“Nashukuru sana Rahimu.”

“Karibu ndani pita,” alinikaribisha kwa furaha zote.

Niliingia koridoni na kupita hadi sebuleni, mke wake aliponiona alizima runinga na kuingia  chumbani kwake.  Rahimu alitikisa kichwa cha masikitiko, akawasha tena runinga na kisha akanichangamkia kwa kuniuliza.

“Eheee! Niambie ndugu yangu unatokea wapi usiku huu? Sio kawaida yako.”

Nilitabasamu kidogo kisha nikamwambia.

“Nina hadithi ndefu sana ya kukupa rafiki yangu lakini siwezi kukuhadithia hapa nyumbani kwako maana hii ni nyumba ya heshima.”

Alicheka kidogo kisha akaniuliza.

“Kwani jambo unalotaka kuniambia si la heshima?”

“Sina maana hiyo Rahimu lakini ni habari za sisi vijana hasa kwa mimi ambaye sina mke, sio hadithi hiyo tu bali kuna nyingine ndani ya hiyo pia.”

“Sawa basi naomba tutoke twende sehemu tulivu tukapate kahawa huku ukinisimulia.”

“Usiku huu Rahimu?”

“Usijali bado mapema Rahimu ndio kwanza saa tatu hii.”

“Na mkeo je, utamwambia unakwenda wapi?”

“Usijali mke wangu huwa anajua nakwenda wapi usiku kama huu.”

“Sawa twende.”

Rahimu alizima runinga, tukatoka nje na kuelekea mtaa wa pili sehemu moja iliyochangamka sana, kukiwa na muziki, vinywaji na vyakula vya kila aina.  Aliagiza nyama choma wakati tukianza na kahawa ya moto sana.

“Ehee! Niambie Rahimu nipe hadithi zote halafu leo nakuona u tofauti kidogo kama una furaha ya mbali sio kama siku zote ambazo majonzi kwako ndio uso wako.”

Nilitabasamu, nikamtazama sana na kumwambia.

“Huwezi amini rafiki yangu leo ni siku ya nne niko hapa jijini.”

“Heeee!! Ulikuwa wapi siku zote hizo, mbona hukuja kwangu, ulikuwa unalala wapi au umepata mwenyeji mwingine?”

“Hapana Besti yangu, ila niliogopa kukusumbua maana umekuwa msaada kwangu hadi nafikia hatua ya kuogopa kwa sababu najishtukia.  Siwezi kukutegemea wewe kila wakati nawe una familia Rahimu.”

“Kwangu ni dhambi kusema hayo rafiki yangu, wewe ni zaidi ya rafiki wala usiohofie hayo. Sasa ulikuwa unalala wapi?”

“Nilikuwa najiegesha chini ya daraja la Savina.”

“Yaani ulikuwa unalala nje Vanuell, ulikuwa umechanganyikiwa?”

“Tuachane na hayo Rahimu tayari yalishapita naomba niongee jambo lililotuleta hapa.”

“Sawa nambie.”

“Baadaya ya kuzunguka sana kila kona ndani ya hili jijini lenu, bila mafanikio, niliamua kuelekea mtaa wa Movan Mero,” niliongea.

Rahimu alishtuka akistaajabu usemi wangu, haraka aliniuliza.

“Movan Mero, umefika mtaa huo?”

“Ndio Rahimu.”

“Umewezaje maana ule ni mtaa ambao hata sisi watu wa Port Villa haturuhusiwi kwenda ni mtaa wa matajiri unaolindwa saa 24.”

Nilitabasamu na kumwongezea mshangao mwingine.

“Nilifanikiwa kupita nikiomba kazi, baadaye kijana mmoja aliniambia kuwa kwa tajiri Alexender Rugoa wanahitaji mfanyakazi wa bustani. Nikaelekea huko na kuruhusiwa kupita.”

“Unanitania Vanuell sio?” aliuliza Rahimu kwa mshangao mkubwa.

“Sikutanii rafiki yangu huo ndio ukweli, kufika ndani nikaambiwa kuna watu wengi sana walikuwa wanakuja kuomba nafasi ya kufanya majaribio tu. Hata hivyo kati ya watu wa tatu waliopita nafasi hiyo na mimi pia nilipata.”

“Hivi Vanuell unaniona mimi mtoto sana wa kuniongopea, wewe upate nafasi ndani ya bustani ya Alexender Rugoa?”

Nini kitafuatia? Usikose kesho.

Tukiwa tunaendelea na simulizi yetu nzuri, hadi hivi sasa umejifunza nini?  


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*