googleAds

Taifa Stars yaungwa mkono kila kona

NA GLORY MLAY

WADAU mbalimbali wa michezo wamejitokeza kuunga mkono timu ya Taifa Stars ambayo ipo nchini Misri kujianda na michuano ya AFCON itakayoanza Ijumaa ijayo. 

Taifa Stars chini ya kocha mkuu Emmanuel Amunike, imepangwa Kundi C pamoja na Algeria, Senegal na Harambee Stars ya Kenya. 

Akizungumza na BINGWA jana, nahodha wa Kagera Sugar, George Kavila, aliweka imani yake na kikosi cha timu ya taifa kilichochaguliwa akisisitiza kitaiwakilisha nchi vyema.

Kavila alisema Watanzania wanatakiwa kumuunga mkono kocha Amunike kwa kazi kubwa aliyoifanya tangu mwanzo hadi kufikia hatua hiyo.

Alisema Mnigeria huyo mwanzoni alikuwa akilaumiwa kwa kufanya vibaya lakini kwa sasa Watanzania wanatakiwa wabadili mitazamo yao na kumsapoti ili naye ajisikie faraja kwa kile ambacho amekuja kukifanya hapa nchini.

“Muda wa lawama umepita, tumuache kocha afanya kile ambacho anaona kwetu Watanzania ni sahihi, tumuunge mkono na tuone ni kwa jinsi gani tutavuka hii hatua na kusonga mbele, tukumbike kuwa hatua tuliofikia ni kubwa sana hivyo tusipende kulaumu… Amunike anauwezo kuliko tunavyofikiria,” alisema Kavila.

Naye kocha mkuu wa Biashara United, Amri Said, alisema michuano ya AFCON ni muhimu kwa taifa hivyo Watanzania wanatakiwa kuacha tofauti zao katika soka na kuwa kitu kimoja.

Said alisema mpaka kufikia hatua hiyo Watanzania wanatakiwa kuhamasika kwa kuona tunashiriki AFCON mwaka huu na siyo kuanza kumlaumu kocha Amunike kwa kikosi alichochagua.

Alisema kikosi kile ni kizuri na kinaleta matumaini makubwa kwa Watanzania hivyo U-Yanga na U-Simba uwekwe pembeni na waangalie kuwamba inayocheza ni Taifa Stars.

“Tuache mambo ya kuongea ovyo, yule ni mwalimu na anajua mpira ni nini, watu wengi wanaongea lakini wengi wao hawajui mpira, hivyo Watanzania wanatakiwa kumsapoti kocha wao ili kuleta mafanikio katika nchi yetu, tuungane kwa pamoja ili kumpa moyo kocha kwa kile anachofanya,” alisema Said.

Katika hatua nyingine, mkufunzi wa timu za vijana, Maalim Saleh, alisema Tanzania ikiachana na mambo ya siasa katika mpira itafikia malengo ambayo wanayataka hususan katika timu ya Taifa Stars.

Saleh alisema watu wengi wanamlaumu kocha kwa kuacha wachezaji wazuri lakini wanasahau jukumu la kocha ni kupanga kikosi anachokihitaji.

“Kocha anaangalia ni mchezaji yupi anajituma katika mazoezi na anafanya vizuri katika timu yake ndiyo anamchagua, tatizo la wachezaji wetu hawana nidhamu na ni wavivu, hawajui kujituma ndiyo maana wanashindwa kuingia katika timu ya taifa,” alisema.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*