Taifa Stars yamtia hofu Mbunge

NA Maregesi paul, Dodoma

MBUNGE wa Kilolo, Venance Mwamoto (CCM), ameonyesha hofu yake juu ya timu ya Taifa ‘Taifa Stars’, hasa wakati huu inapoelekea kwenye maandalizi ya Kombe la Afrika (AFCON), nchini Misri, Julai mwaka huu.

Stars ilifuzu kushiriki michuani hiyo Machi 24 mwaka huu, ilipoitandika Uganda bao 3-0, katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Mwamoto aliyasema hayo wakati akichangia bajeti ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa mwaka wa fedha 2019/20 bungeni jijini Dodoma jana.

Alisema Timu ya Taifa haifanyi vizuri kwa sababu kilabu nyingi zimesheheni wachezaji wa kigeni, ambao wengi uwezo wao unafanana na wachezaji tulionao Tanzania.

“Mfano klabu ya Simba wachezaji watatu tu ndio wanajitahidi, kuna Meddie Kagere, Emmanuel Okwi na Clatous Chama na Yanga mchezaji mmoja tu.

“Nahofia uimara wa timu ya soka ya Taifa ‘Taifa Stars’ kwa kuwa klabu nyingi nchini zina wachezaji wengi wa kigeni ambao uwezo wao ni mdogo, kutokana na hali hii, kuna haja ya Serikali kuweka masharti kwamba, ili kumsajili mchezaji wa kigeni nchini, lazima awe anachezea timu ya taifa ya nchi yake.

Pia iwekwe sheria kubana klabu za ndani zisisajili wachezaji wengi wa nje, kwasababu wanawabana wachezaji wa ndani wasipate nafasi ya kucheza, hivyo kuidhoofisha timu ya Taifa,” alisema.

Hata hivyo, Shirikisho la Soka nchini (TFF), tayari lilipitisha idadi ya wachezaji 10 wa kigeni kusajiliwa kwenye timu.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*