TAIFA STARS TUPENI BURUDANI

KIKOSI cha Taifa Stars kitashuka kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam leo kucheza na Cape Verde katika mchezo wa marudiano wa kuwania kufuzu fainali za Afrika (Afcon), zitakazochezwa mwakani nchini Cameroon.

Taifa Stars wanatakiwa kutupa burudani Watanzania kwa kuibuka na ushindi mnono, baada ya wiki iliyopita kuwakosesha furaha kutokana na matokeo ya kufungwa mabao 3-0 na Cape Verde katika mchezo wa kwanza uliochezwa kwenye uwanja wao wa nyumbani.

Tanzania ambayo ipo Kundi L pamoja na Uganda, Lesotho na Cape Verde, ina kila sababu ya kushinda mchezo wa leo kwa kuwa nao watakuwa nyumbani wakicheza mbele ya mashabiki wao.

Tunaamini kwamba, Taifa Stars haitafanya makosa kwa Cape Verde, kwani matarajio yetu ni ushindi katika mchezo wa leo na si vinginevyo.

BINGWA tunaamini kwamba vijana wa Taifa Stars watafanya kile Watanzania wanahitaji kutoka kwao, kwani wamechoka na kuwa wasindikizaji katika michuano ya kimataifa.

Tunasema pamoja na kwamba mpira ni dakika 90, lakini Taifa Stars iwe na kazi moja ya kuibuka na ushindi, ambao utarejesha matumaini ya kufuzu fainali za mwakani.

Hivyo, tunaamini kwamba benchi la ufundi la Taifa Stars limefanya maboresho katika kikosi hicho ili kuweza kupata matokeo mazuri katika mchezo wa leo na ule utakaofuata dhidi ya Lesotho na Uganda.

BINGWA tunasema kwamba, Watanzania wajitokeze kwa wingi uwanjani kuishangilia timu yetu ya Taifa Stars ikiwa ni sehemu yao ya kuisaidia timu hiyo.

Tunaamini kwamba Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Serikali na wadau wengine wametimiza majukumu yao na kilichobaki ni mashabiki kwenda uwanjani kuishangilia Taifa Stars.

Tunasema timu ya Cape Verde inafungika na hakuna haja ya kuihofia  kutokana na matokeo yaliyopita.

Kwa upande wetu BINGWA tutakuwa wa kwanza kwenda kuisapoti timu hiyo ili iweze kupata matokeo mzuri,  mwakani Taifa Stars iwe ni miongoni mwa timu zitakazoshiriki fainali za Afcon.

Tunaitakia kila la heri Taifa Stars


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*