TAIFA STARS ISIVUNJIKE MOYO

WIKI iliyopita, timu ya Tanzania, Taifa Stars, ilipoteza mchezo wa kuwania kufuzu fainali za Afrika (Afcon) zitakazochezwa mwakani nchini Cameroon, baada ya kufungwa mabao 3-0 na Cape Verde.

Tanzania ambayo ipo Kundi L pamoja na Uganda, Lesotho na Cape Verde, kutokana na matokeo hayo, ipo katika mazingira magumu ya kufuzu fainali hizo.

Katika kundi hilo, Uganda wanaongoza kutokana na pointi saba wakifuatiwa na Cape Verde wenye pointi nne, Lesotho na Tanzania  wana pointi mbili.

Kwa matokeo hayo, Tanzania inahitaji kushinda michezo yote mitatu iliyosalia ili iweze kufuzu fainali za mwakani.

Tunaamini hilo linawezekana kwa Tanzania  kushinda ikijipanga vizuri, kuanzia mchezo wa marudiano dhidi ya Cape Verde uliopangwa kuchezwa kesho kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Katika soka tunaamini kwamba, timu pinzani inafungwa kutokana na makosa, hivyo Tanzania ikiyafanyia kazi makosa yaliyojitokeza katika mchezo uliopita dhidi ya Cape Verde, inaweza kujiweka kwenye mazingira bora ya kushinda michezo yote na kufuzu fainali hizo.

Tunasema kwamba, matokeo ya kufungwa na Cape Verde yasiwakatishe tamaa wachezaji, benchi la ufundi na Watanzania kwa ujumla, kwani soka lina matokeo matatu; kushinda, kufungwa na sare.

Hivyo, tunaamini benchi la ufundi la Taifa Stars litafanya maboresho katika kikosi hicho ili kupata matokeo mazuri katika michezo itakayofuata.

BINGWA tunasema kwamba, Watanzania waendelee kuzungumza lugha moja ya kuisaidia timu yetu ya Taifa Stars kufanya vizuri kwa michezo iliyosalia, kwani katika soka tunaamini lolote linaweza kutokea ndani ya dakika 90.

Tunasema kufungwa na Cape Verde isiwe sababu ya kuacha kusaidia timu yetu kwa kuona haina nafasi ya kufuzu fainali hizo, kwa kuwa bado kuna dakika 270 za kuweza kuamua matokeo.

Kwa upande wetu, BINGWA tunaamini sapoti ya Watanzania  kwa timu yao itaanza kesho wakati  itakaposhuka Uwanja wa Taifa kurudiana na Cape Verde, kwani matokeo bora yanaweza kurejesha matumaini ya kusonga mbele.

Tunaitakia kila la heri Taifa Stars.

 


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*