Sylvia asitelekezwe Miss World 2019

MISS Tanzania 2019, Sylvia Sebastian kutoka Mwanza, anatarajiwa kuipeperusha Bendera ya Tanzania fainali za 69 za Miss World zinazotarajiwa kufanyika Desemba 14, mwaka huu kwenye ukumbi wa ExCeL, jijini London, Uingereza.

Fainali za Miss World mwaka huu zinatarajiwa kushirikisha warembo zaidi ya 100 kuwania taji linaloshikiliwa na Vanessa Ponce wa Mexico.  

Ikumbukwe kuwa Sylvia, alitwaa taji la Miss Tanzania baada ya kuwashinda wenzake 19 katika kinyang’anyiro kilichofanyika kwenye ukumbi wa Millennium Tower, Dar es Salaam mwezi uliopita.

Nafasi ya pili katika shindano hilo, ilikwenda kwa binti kutoka Kinondoni, Queenmugesi Ainory, wakati mshindi wa tatu akiwa ni Queen Magese (Kinondoni), nafasi ya nne ikichukuliwa na Greatness Nkuba (Pwani), huku Susan Faustine (Shinyanga) akiwa wa tano.

Akizungumza baada ta kutangazwa mshindi wa taji hilo, Sylvia alisema: “Ninafurahi kupata nafasi hii adhimu, sikutegemea, naomba wadau na Watanzania kunipa ushirikiano kipindi hiki ninachoanza kujiandaa na mashindano ya Dunia.” 

Sylvia aliahidi kuiwakilisha Tanzania ipasavyo katika kinyang’anyiro cha Miss World, akiwataka wadau wa urembo na watanzania kwa ujumla kumpa sapoti katika maandalizi yake.

Na sasa Sylvia anajiandaa kwa ajili ya kwenda kufanya kweli Miss World, kuona kama anaweza kufikia au kuzidi mafanikio ya Nancy Sumari aliyeibuka Mrembo Bora wa Dunia wa Afrika mwaka 2005 (Miss World Africa 2015). 

Tukiwa kama miongoni mwa wadau wa mashindano ya urembo nchini, BINGWA tunadhani kipindi hiki ni muhimu mno kwa wadau kumuunga mkono Sylvia katika maandalizi yake.

Kuelekea ushiriki wake Miss World, tunadhani ni vema Sylvia akaandaliwa ipasavyo ili aweze kwenda kuipeperusha vema Bendera ya Tanzania huko London.

Tunadhani jukumu la kumwandaa Sylvia, lisibaki kwa mratibu wa shindano la Miss Tanzania, Basila Mwanukuzi pekee, bali kila mmoja, ikiwamo Serikali, ione ni kwa vipi anaweza kutoa mchango wake ili kumwezesha binti yetu huyo kwenda kufanya kweli London.

Kama kila mmoja wetu anavyofahamu, fainali za Miss World ni fursa ya kipekee kwa washiriki kuyatangaza mataifa yao kwani wawapo huko, huwa hawatambuliki kwa majina yao binafsi, zaidi ya yale ya nchi zao.

BINGWA tunamtakia kila la kheri Sylvia katika maandalizi yake ya kuelekea Miss World, tukiamini atapewa kila sapoti inayostahili ili angalau aweze kufuata nyayo za Nancy Sumari au hata kumzidi.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*