Suluhisho tatizo la viungo Liverpool hili hapa

MERSEYSIDE, England

BAADA ya Liverpool kukubali kichapo cha mabao 2-1 kutoka kwa PSG, katika mchezo wa tano hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Ulaya uliochezwa wiki iliyopita, Jurgen Klopp, aliombwa kuizungumzia safu ya viungo katika timu yake.

Mwandishi wa habari alimuuliza kocha huyo wa Liverpool swali, iwapo anahisi kuna tatizo lolote kwenye safu yake ya viungo iliyoonekana kuzidiwa na viungo wa PSG.

Klopp alimjibu hivi mwandishi yule: “Kwenye ligi msimu huu tumefungwa mabao si zaidi ya matano, ila wewe leo unaniuliza viungo wangu walizidiwa?”

Hilo ndilo lilikuwa jibu la Klopp ambaye alionesha wazi kukerwa na swali hilo na aliongeza: “Sijaliona hilo tatizo unalolizungumzia. Tungeweza kufunga mabao zaidi kwa jinsi tulivyojitahidi kutengeneza nafasi, lakini niwe mkweli, sijaona tatizo kwa viungo wangu.”

Hata hivyo, safu hiyo ya viungo wa Liverpool ambao walianza dhidi ya PSG, ndiyo ile ile iliyochuana na Real Madrid katika fainali ya Ligi ya Mabingwa msimu uliopita.

Viungo hao walikuwa ni nahodha, Jordan Henderson, Giorginio Wijnaldum na mkongwe, James Milner, hivyo madai ya Klopp kwamba hakuona matatizo au mapungufu kwa viungo hao, yalishangaza.

Ikumbukwe kocha huyo aliamua kuingiza sura mpya kwenye safu hiyo kwa kuwasajili Fabinho, Naby Keita na pia alimtaka sana kiungo mshambuliaji wa Lyon, Nabil Fekir.

Klopp alidhihirisha kwamba alitaka kuiona timu yake ikiuanza msimu na nguvu mpya katikati ya uwanja.

Lakini siku zote inatambulika vitendo vina nguvu zaidi kuliko maneno. Kauli ya Klopp bado haitabadilisha ukweli ambao hata yeye anaufahamu.

Ni sawa na msimu uliopita alivyokuwa akimtetea mlinda mlango, Loris Karius, lakini alipoiona fursa ya kuongeza nguvu langoni, alimsajili Mbrazil, Alisson Becker, kutoka AS Roma.

Tatizo linaanzia wapi?

Takwimu zinaonesha kwamba, kichapo ambacho Liverpool ilikipata dhidi ya PSG, kilikuwa ni cha tano mfululizo katika michezo iliyocheza ugenini, ukiwemo wa nusu fainali dhidi ya Roma na fainali zote za msimu uliopita.

Milner na Wijnaldum walianza katika mechi hizo tano sambamba na nahodha wao, Henderson, kwenye safu ya viungo watatu halafu Liverpool ikaja kupoteza nyumbani kwa Napoli msimu huu, mechi ambayo Keita alianza lakini akatoka mapema baada ya kuumia.

Katika mechi tatu za msimu huu ambazo Liverpool imepoteza Ulaya, timu hiyo imeweza kupiga jumla ya mashuti manne tu yaliyotokana na shambulizi la kawaida, mashuti yote yakipatikana katika mechi moja dhidi ya Red Star Belgrade.

Takwimu hiyo ni kama inaendana na hii ambayo Henderson, Milner na Wijnaldum, walifunga mabao manne tu kati yao, katika mechi 148 walizocheza msimu uliopita.

Tatizo lenyewe linaanzia hapa; wakati Mohamed Salah, Sadio Mane na Roberto Firmino, hawafungi mabao, ni ngumu kuona wachezaji wengine wa Liverpool wakiisaidia timu yao katika suala la kutikisa nyavu.

Mashabiki wengi wa Liverpool wanafahamu kuwa Milner, Henderson na Wijnaldum, ni viungo wanaocheza soka la aina moja.

Hawana ubunifu wa kutosha na nguvu ya kupachika mabao, tofauti na wachezaji wa timu nyingi za ubingwa wanavyokuwa na vitu vingi kuliko wanavyoweza kuchangia kwa wakati husika.

Takwimu zinaonesha kuwa, viungo hao pia wamekuwa na mchango mdogo kwenye upatikanaji wa pointi, ambapo kila wanapocheza pamoja wana wastani wa kuchangia pointi 1.66 kwa mechi, sawa na pointi 63 kwa msimu mzima.

Hiyo ndiyo takwimu inayobeba hoja ya wengi wanaoamini safu ya viungo Milner, Henderson na Wijnaldum, ni ile inayopaswa kuwa kwenye timu za chini, kwani hawana msaada wa kutosha kwa washambuliaji.

Liver inawakosa hawa

Msimu uliopita, viungo walioongoza kwa kufunga mabao Liverpool walikuwa ni Alex Oxlade-Chamberlain, Philippe Coutinho na Emre Can. Lakini wawili hawapo tena, mmoja anaumwa. Na licha ya kuwasajili Keita na Fabinho, Klopp ameendelea kuwaamini viungo wachovu.

Coutinho alikuwa ni mchezaji muhimu sana katika nusu ya kwanza ya msimu wa 2017/18. Alikuwa na ubunifu wa hali ya juu akicheza kama mmoja wa viungo watatu au kushoto sambamba na washambuliaji.

Baada ya kuondoka kwake, mapema Januari mwaka huu,  Oxlade-Chamberlain, akakabidhiwa mikoba yake na kufanya vyema, lakini alivyoumia tu, ukaonekana udhaifu mkubwa kwa viungo waliobakia ambao wameonesha wazi hawana uwezo kuwachezesha washambuliaji.

Udhaifu huo ndio ukamfanya Klopp amsajili Xherdan Shaqiri. Lakini, baada ya kumtumia kama kiungo mshambuliaji dhidi ya Southampton na kumtoa kipindi cha pili baada ya kufanya vizuri mno, Klopp alianza kumtumia kama kiungo wa kulia.

Matamanio makubwa ya Klopp ni kumtumia Shaqiri katikati, lakini bado hajamwamini vya kutosha. Hivyo imembidi abadilishe muundo wa kikosi kutoka 4-3-3 hadi 4-2-3-1, akimchezesha Salah kama namba tisa na kumshusha Roberto Firmino namba 10.

Ni wazi alitaka kutumia muundo huo ambao aliwahi kuutumia Dortmund na ukampa mafanikio, kwa ajili ya Fekir acheze namba 10 na Shaqiri awe msaidizi wake kutokea benchi.

Suluhisho?

Kitendo cha Klopp kumsajili Shaqiri kilikuwa na maana kubwa, lakini bado haiwezi kusahaulisha kushuka kwa kasi ya washambuliaji wa Liverpool katika kipindi cha hivi karibuni, hasa Firmino na Salah.

Labda ni wakati mwafaka wa Klopp kufanya mabadiliko ya muda mfupi, kwa kurudisha muundo wa 4-3-3, ili aweze kuwatumia washambuliaji wake watatu kama kawaida na pia aweze kuwafanyia mabadiliko (rotation) kulingana na mechi.

Kwa mfano, safu ya viungo Fabinho, Wijnaldum na Keita itaifanya Liverpool icheze kwa mzani ulio sawa tofauti na ‘kombinesheni’ ya Henderson, Wijnaldum na Milner.

Lakini Klopp anaonekana kumwamini zaidi Fabinho katika safu ya viungo wawili, ambayo alifanya vizuri mno alivyoanzishwa dhidi ya Red Star kwenye mchezo uliochezwa Anfield na Liverpool kushinda mabao 4-0.

Hiyo ni nafasi ambayo Henderson imemshinda tangu enzi za Brendan Rodgers, kabla ya kubadilishiwa nafasi na kucheza pembeni hivyo nahodha wake, Steven Gerrard, akaachiwa awe kiungo wa chini.

Ni wazi Klopp ana kazi nguvu hivi sasa, labda ndiyo itakuwa hivyo hadi mwakani, ambapo Keita na Fabinho watakuwa wametulia vya kutosha na pia usajili mpya ukafanyika.

Suluhisho la muda mrefu ni Klopp kuendelea na muundo wa 4-2-3-1, lakini awatumie Fabinho na Keita katika safu ya viungo wawili. Ikumbukwe nyota hao walikuwa wakitumika hivyo katika timu walizotoka na wana ubora unaolingana.

Fabinho ni kiungo mzuri wa kukaba, Keita ni msaidizi mzuri wa kushambulia (box-to-box midfielder).

Pia, kama Liverpool watasajili namba 10 ina maana Firmino atarudi kwenye nafasi yake kama namba tisa ambayo ilimng’arisha msimu uliopita na pia Salah atarudi kwenye winga ya kulia ambayo ilimfanya avunje rekodi za mabao Anfield.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*