Straika Olunga adai hana presha

PARIS, Ufaransa

MSHAMBULIAJI tegemeo wa timu ya taifa ya Kenya, Harambee Stars, Michael Olunga, amesema hana presha ya aina yoyote timu ikijiandaa na michuano ya Kombe la Afrika nchini Misri.

Harambee Stars inatarajia kucheza mchezo wa kimataifa wa kirafiki dhidi ya Jahmuri ya Kidemokrasia ya Congo Juni 15 kabla kocha Sebastien Migne hajataja kikosi chake cha mwisho.

Olunga ambaye ni mrefu kwa kimo na anachezea Kashiwa Reysol ya Japan ni tegemeo kwa kocha ya Migne kwa kikosi cha Harambee Stars kinachorudi kwenye michuano hiyo baada ya kuikosa kwa miaka 15.

Macho yote yatakuwa kwa Olunga baada ya kocha Migne kumtema Allan Wanga aliyefunga mabao 18 msimu wa Ligi Kuu Kenya uliomalizika hivi karibuni na Jesse Were ambaye amekuwa na msimu mzuri na timu yake ya Zesco United kutoka Zambia.

Hata hivyo Olunga amesisitiza katika mazoezi wanayofanya, timu haitegemei staili ya mchezaji moja mabali wanataka kucheza kama timu.

“Sina presha yoyote kwasababu mwisho wa siku kitu muhimu ni kucheza kama timu na kama nitapewa nafasi nitajitolea kwa moyo wote kwasababu mimi ni mzalendo kwa nchi yangu,” alisema Olunga akiwa kambi ya timu ya taifa iliyopo Ufaransa.

“Imekuwa safari ndefu kwa timu kufika hapa na tutakapokanyaga uwanjani kwa ajili ya mechi yetu ya ufunguzi, tutafanya kile tuwezalo kufurahisha Wakenya.

“Naamini sasa hivi kila mtu katika kambi hii anayo ndoto kwasababu hakuna hata mchezaji moja alishawahi kucheza kwenye michuano hii mimi nikiwa moja wao, na kila mtu amedhamiria kwenda kuonyesha ubora wa kiwango chake.”

Kenya itaikabili Algeria katika mechi ya ufunguzi Kundi C Juni 30 kwenye Uwanja wa June 30 kabla ya kuivaa Taifa Stars ya Tanzania na kucheza mechi ya mwisho hatua ya makundi dhidi ya Senegal. 


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*