googleAds

Straika Okwi mtu mbaya

NA MAREGES NYAMAKA

MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba, jana waliendeleza ubabe katika Uwanja wa Sokoine, Mbeya, baada ya kuwachapa wenyeji wao Tanzania Prisons bao 1-0, katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara.

Ushindi huo umeiwezesha Simba kufikisha pointi 78 baada ya kushuka dimbani mara 30, ikishinda michezo 24, sare tatu na kufungwa miwili.

Wekundu hao wa Msimbazi wapo nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi hiyo wakiwa na tofauti ya pointi mbili nyuma ya vinara Yanga, huku Azam FC wakishika nafasi ya tatu.

Bao pekee lililowapa ushindi muhimu Simba lilifungwa na straika Mganda, Emmanuel Okwi, dakika ya 11 hivyo kufanikisha lengo lao la kuvuna pointi zote sita katika dimba la Sokoine, awali wakiifunga Mbeya City mabao 2-1.

Okwi alifunga bao hilo kwa shuti kali lililozama moja kwa moja wavuni baada ya kipa wa Prisons, Aaron Kalambo, kutoka langoni kufuata mpira lakini akashindwa kuuzuia.

Dakika ya 15, Okwi alipaisha juu mpira wa kichwa alioupiga akiunganisha krosi ya Zana Coulibally kabla ya Clatous Chama kupoteza nafasi ya wazi dakika ya 31 akiwa ndani ya eneo la hatari.

Okwi aliyekuwa mwiba langoni mwa Prisons, alikosa bao dakika ya 38 baada shuti lake la mpira wa adhabu aliopiga akiwa nje kidogo ya 18 kupaa juu ya lango.

Hata hivyo, Prisons walifurukuta na kufanya shambulizi kupitia kwa Ramadhani Ibata dakika chache kabla ya mapumziko, lakini halikuzaa matunda baada ya shuti hilo kudakwa na kipa, Aishi Manula.

Simba waliendeleza kasi yao kipindi cha pili na dakika ya 61, Okwi alikosa nafasi baada ya kuanguka ndani ya eneo la hatari, huku Meddie Kagere naye akikosa bao dakika ya 66 kwa kushindwa kumalizia krosi ya Haruna Niyonzima.

Mashambulizi mengi ya Prisons yaliyokuwa yakielekezwa langoni mwa Simba yalizuiliwa na Yussuf Mlipili sambamba na pacha wake, Erasto Nyoni, waliosimama vyema katika eneo la ulinzi.

Dakika ya 87, Adama Adam wa Prisons alifumua shuti ambalo hata hivyo lilikosa mwelekeo akitumia makosa ya  Coulibally aliyerudisha mpira nyuma na kunaswa na straika huyo.

Prisons walifanya shambulizi jingine dakika moja baadaye lililotokana na shuti la Jumanne Nimkaza, lakini likapanguliwa na Manula.

Dakika ya 89, Chama alikosa nafasi ya wazi baada kushindwa kuiunganisha vizuri pasi ya Kagere.

PRISONS: Aron Kalambo, Michael Mpasa, Leon Mutalemwa, Nurdin Chona, Vedastus Mwihambi, Jumanne Nimkaza, Salum Kimenya/Cleofance Mkandala(dk70), Ezekia Mwashilindi, Adama Adam, Ramadhani Ibata na Ismail Kada.

SIMBA: Aishi Manula, Zana Coulibally, Mohamed Hussein, Yussuf Mlipili, Erasto Nyoni, James Kotei, Clatous Chama, Mzamiru Yassin, Meddie Kagere, Emmanuel Okwi/Jonas Mkude(dk67) na Haruna Niyonzima/Hassan Dilunga(dk80).


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*