STRAIKA AKATAA MAMILIONI YA SIMBA

NA ZAINA IDDY

WAKATI wachezaji wengi wakisaka nafasi ya kuchezea timu kongwe hapa nchini, Simba na Yanga, hali imekuwa tofauti kwa straika,  Kelvin Sabato, aliyegomea kuchukua Sh milioni 13, zikiwa ni sehemu ya usajili wake katika klabu ya Simba.

Simba walianza kufukuzia saini ya Sabato aliyefanikiwa kufunga ‘hat-trick’ katika mchezo wa mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu Tanzania Bara, akiwa na kikosi cha Stand United.

Kamati ya usajili ya Simba inayoongozwa na Mwenyekiti, Zakaria Hans Pope, ilitaka kusajili straika huyo ili kutimiza matakwa ya kocha mkuu wa timu hiyo, Joseph Omog,  kupendekeza aongezewe straika mzawa mmoja katika usajili wa dirisha dogo wa ligi linalotarajia kufungwa leo usiku.

Hata hivyo, straika huyo ameitolea nje Simba na kwenda kujiunga na Majimaji waliofikia dau la Sh milioni saba kwa mkataba wa miezi sita.

Pamoja na Simba kukutana na straika na meneja wake juzi mchana kwa lengo la kuvunja mkataba waliopewa na Majimaji, harakati hizo hazikuweza kufanikiwa.

Akizungumza na BINGWA juzi, Sabato alisema hakuona umuhimu wa kusaini Simba kwa dau dogo la Sh milioni 13 kwa kipindi cha miezi 18.

“Jana (juzi) tulikutana na uongozi wa Simba ambao waliniambia nivunje mkataba na Majimaji kwa kuwarudishia fedha zao ambazo wao wamenipa.

“Ningeweza kwenda iwapo kama muda huo waliotaka kunipa wangenipa Sh milioni 40 na si milioni 13 ambazo kwangu si kitu cha ajabu sana ukizingatia nina mipango yangu mingi inayoweza kuja kuniingizia fedha pasipo kuniathiri utendaji wangu wa kazi,” alisema.

Straika huyo amejiunga na Majimaji akiamini atapata nafasi ya kucheza na kukuza kipaji chake kuliko kwenda Simba ambako hana uhakika wa kupata namba ya kudumu kutokana na ushindani katika idara anayocheza.

 


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*