googleAds

STARS PIGA HAO CAPE VERDE

NA MWAMVITA MTANDA           |      


 

TIMU ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, inatarajia kushuka dimbani leo kukabiliana na Cape Verde katika mchezo wa kuwania tiketi ya kufuzu fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON), kwenye Uwanja wa Kimataifa wa Cape Verde.

Mchezo huo utakaoanza saa 10:00 jioni, unatarajiwa kuwa na upinzani mkubwa, kwani kila timu ina nafasi ya kufuzu fainali hizo za mwakani zitakazofanyika nchini Cameroon.

Katika mchezo uliopita wa fainali hizo, Stars walicheza na Uganda mwezi uliopita na kupata suluhu ugenini, matokea yaliyopokewa kwa shangwe mno na mashabiki wa soka hapa nchini.

Kwa upande wa Cape Verde, walipata sare ya bao 1-1 dhidi ya Lesotho, hivyo leo hawatakuwa tayari kupoteza mchezo huo wakiwa kwenye uwanja wao wa nyumbani.

Akizungumza na BINGWA jana kwa mtandao kutoka Cape Verde, Kocha Mkuu wa Stars, Emmanuel

Amunike, alisema kuwa, kikosi chake kimetua salama nchini humo na wamefanikiwa kufanya mazoezi jana katika uwanja huo.

“Tunashukuru Mungu tumefika salama na kikosi kipo salama, tumefanya mazoezi leo (jana) katika Uwanja wa Kimataifa wa Cape Verde ili kuwafanya vijana kuutambua uwanja watakaoutumia,” alisema Amunike.

Amunike alisema kuwa, hali ya uwanja huo ni nzuri, japo kuna baridi ambayo alisema ni rafiki kwa mchezaji kufanya misuli isichoke kwa haraka anapokuwa uwanjani.

Kocha huyo alisema kuwa, kutokana na ubora wa kikosi chake, kuna uwezokano mkubwa wa kurudi na ushindi, kwa kuwa amewaandaa kwa kiwango cha kimataifa, ukizingatia ana wachezaji ambao tayari wameshakabiliana na mechi ngumu zaidi ya hiyo ya Cape Verde.

“Sitafurahi kuona tunapoteza nafasi hii adimu ambayo nchi nyingi zilitamani kushiriki, lakini zilishindwa kwasababu nyingine, nitahakikisha kuwa ninasimamia mpaka tunafanikiwa kufuzu fainali hizo za mwakani,” alisema Amunike.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*