‘STARBOY MORATA’ SHIDA SI KUTOFUNGA NA MIGUU, SHIDA INAANZIA KWA CHELSEA NZIMA

LONDON, England

KAMA mchezo wa soka ungekuwa unaitwa ‘mpira wa vichwa’, basi Alvaro Morata bila shaka angekuwa mshambuliaji bora wa mchezo huo.

Mhispania huyo anayeitumikia klabu ya Chelsea, si kwamba ni straika mbovu kwenye soka, ni mzuri lakini hiki anachokionesha msimu huu cha kuonesha makali ya kufunga mabao kwa kichwa kuliko miguu, ndicho kilichowakera sana mashabiki wa Chelsea baada ya sare ya mabao 2-2 dhidi ya Arsenal.

Morata alipata nafasi nyingi, tena nzuri mno za kufunga mabao kwa upande wa timu yake ya Chelsea, lakini alishindwa kuzitikisa nyavu za Arsenal.

Adui wa kwanza wa Morata kwenye mchezo huo uliochezwa mapema wiki hii kwenye dimba la Emirates alikuwa ni Petr Cech na wa pili alikuwa ni yeye mwenyewe.

Iwapo angetumia vyema nafasi hizo, Morata angeifanya timu yake iondoke na ushindi mnono katika mtanange huo na angeisaidia sana Chelsea katika harakati za kuisaka nafasi ya pili wikiendi ijayo watakapoingia tena dimbani kucheza mechi ya Premier League.

Baada ya kuuzungumzia mwenendo wake wa ufungaji mabao msimu huu, tuzitazame takwimu zake zinasemaje kulinganisha na washambuliaji wengine bora msimu huu ndani ya Premier League.

Mshambuliaji huyo wa zamani wa Real Madrid na Juventus ana jumla ya mabao 10 msimu huu, sawa na Romelu Lukaku lakini akiachwa mbali na akina Harry Kane (18), Mohamed Salah (17), Raheem Sterling (14) na Sergio Aguero (13).

Lakini, hebu tufahamu kwa undani zaidi namna mastraika hao walivyofunga mabao yao hayo? Na ni baada ya kujaribu mara ngapi katika mechi walizocheza?

Kwa msaada wa mtandao wa takwimu wa ‘Opta’, takwimu zote hizi hapa.

 

Kwa mguu wa kulia

Sterling: 29.4% – (mabao 10 katika mashuti 34).

Salah: 22.2% – (mabao mawili katika mashuti tisa).

Aguero: 20.9% – (mabao tisa katika mashuti 43).

Lukaku: 18.2% – (mabao mawili katika mashuti 11)

Kane: 9.9% – (mabao saba katika mashuti 71)

Morata: 9.7% – (mabao matatu 3 katika mashuti 31)

 

Takwimu hizo zinaonesha kuwa Morata ameonesha uwezo mdogo sana wa kufunga mabao mengi kwa mguu wenye nguvu zaidi katika mashuti yote aliyojaribu.

Amemzidi hata Kane ambaye hata hivyo, amejaribu mashuti 40 zaidi yake.

 

Kwa mguu wa kushoto

Kane: 29.6% – (mabao nane katika mashuti 27)

Sterling: 22.2% – (mabao manne katika mashuti 18)

Salah: 20.9% – (mabao 14 katika mashuti 67)

Lukaku: 14.3% – (mabao matano katika mashuti 35)

Morata: 11.1% – (bao 1 katika mashuti tisa)

Aguero: 0% – (hana bao katika mashuti 12)

 

Hapa tunaona kuwa ni Aguero pekee ambaye hajafunga bao kwa kutumia mguu wake wa kushoto, na ndiye straika mbovu katika hilo eneo, anayemfuatia kwa ukaribu ni Morata.

Na sasa tuelekee kwenye eneo ambalo ulilisubiri kwa hamu kuona takwimu zake zilivyo…

 

Kwa kutumia kichwa

Aguero: 33.3% – (mabao manne katika vichwa 12)

Morata: 31.6% – (mabao sita katika vichwa 19)

Lukaku: 20% – (mabao matatu katika vichwa 15)

Kane: 16.7% – (mabao matatu katika vichwa 18)

Salah: 16.7% – (bao moja katika vichwa 6)

Sterling: 0% – (hana bao katika kichwa kimoja alichojaribu)

 

Kama ulivyotegemea kuona, Morata kwenye eneo hilo ametisha sana msimu huu, lakini cha kushangaza  Aguero ana asilimia nzuri ya kufunga mabao katika vichwa alivyojaribu kuliko Morata.

Na shida moja tu iliyosababisha Morata asiongoze ni kwamba, nyota wenzake ndani ya klabu ya Chelsea hawajakaza kamba za viatu vyao na kumimina krosi za kutosha ambazo zikitua juu ya kichwa cha Mhispania huyo basi hesabu goli.

Bila shaka hii kesi tumeimaliza.

Ili kumfanya Morata atoe upinzani mkali kwenye vita ya kuwania kiatu cha dhahabu Premier League au kuwapa mataji, basi watambue nguvu yake ya kutupia mabao ipo kichwani, cha msingi zimiminwe krosi zilizokwenda shule tu. Hivyo tu.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*