SOURFA kuanzisha soka la vijana, wanawake Unguja

NA IBRAHIM MAKAME, ZANZIBAR

KAMATI ya Utendaji ya Chama cha Soka Mkoa wa Kusini Unguja (SOURFA), imekutana kwa mara ya kwanza jana, tangu kuchaguliwa kwake Aprili 12, mwaka huu na kuazimia kuanzisha soka la vijana na wanawake.

Kikao hicho kilichoongozwa na mwenyekiti wake, Shauri Hassan Juku, kilifanyika jana asubuhi kwenye Ukumbi wa Shule ya Kibele, visiwani hapa.

Akizungumza na BINGWA jana, Makamu Mwenyekiti wa chama hicho, Abubakar Khatib Kisandu, alisema lengo la kikao hicho lilikuwa ni kukabidhiana majukumu ya kazi.

Kisandu alisema kikao hicho pia kilijadili masuala mbalimbali, ikiwamo mipango  ya maendeleo ya chama hicho.

Alisema waliweza kujadili namna ya kuendesha michuano ya wilaya na mkoa.

Kisandu alisema kikao hicho kiliunda kamati mbalimbali za michuano za mkoa huo.

Alisema wajumbe wa kikao hicho walipitisha malengo makuu, yakiwamo kuanzisha soka la vijana na wanawake ambalo limekuwa ni changamoto kubwa kwa Mkoa wa Kusini Unguja, ili kuweka misingi imara ya soka.

‘’Tunaomba ushirikiano na wadau wa mpira wa Mkoa wa Kusini Unguja kwa lengo la kuona tunafanya bidii kubwa ili kuwa na soka la vijana na wanawake kuanzia ngazi za vijana,’’ alisema Kisandu.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*