Souness aeleza ukweli wa Man Utd ya miaka ijayo

MANCHESTER, England

MKONGWE wa zamani wa timu ya Liverpool, Graeme Souness, anaamini kuwa itapita misimu kadhaa ya usajili ambayo klabu ya Manchester United itatumia fedha nyingi mno kutengeneza timu ya kutwaa mataji.

Kauli hiyo ya Souness imekuja baada ya kushuhudia mashetani wekundu hao waking’olewa na Barcelona kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya mapema wiki hii kwa jumla ya mabao 4-0.

Kwa mujibu wa mchambuzi huyo wa soka, wachezaji wengi wanaoitumikia United ni aidha wana uwezo usiojitosheleza au wasio na hadhi ya kuendelea kuwepo Old Trafford.

Kama hiyo haitoshi, Souness alidai kuwa hajashawishika na Ole Gunnar Solskjaer kuwa ndiye kocha atakayefaa kudumu Man Utd kwa muda mrefu.

“Solskjaer na Man Utd kwa ujumla watahitaji muda mrefu wa kujisuka upya. Hakuna njia ya mkato itakayowapa mafanikio. Nazungumza kama mtu wa soka, kibarua alichokipata Ole ni kizito,” alisema Souness.

“Man Utd itahitaji wachezaji wengi bora zaidi ya vijana wao kutoka akademi, United wanahitaji nyota katika soko la usajili. Si kwa mwaka mmoja, bali ni miaka kadhaa inayokuja.

“Makocha waliopita hawakufanya sajili za kueleweka sana. Ili Man Utd wanase mafanikio wakiwa na Solskjaer, wanatakiwa kubadilisha namna wanavyofanya usajili.

“Wachezaji waliocheza dhidi ya Barcelona hawana hadhi ya kuendelea kuwepo pale kwa miaka minne hadi mitano kuanzia sasa. Tofauti na hapo, itabidi tusubiri kama watapandisha viwango vyao na kuwa wachezaji muhimu zaidi kwa United,” alisema.

Aidha, Souness aliongeza kuwa, kutokana na presha kubwa ya United kurudi kwenye mstari na kushinda mataji kama zamani, huenda wakaingia kwenye mtego wa kutumia mamilioni ya pauni katika soko la usajili, japo wanaweza pia wasifanye hivyo.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*