SOMA HIYOOO Ubingwa Ligi ya Mabingwa Ulaya unatua huku

GENEVA, Uswisi

NI timu nane ndizo zilizobaki kuelekea ukingoni mwa msimu huu wa Ligi ya Mabingwa Ulaya, michuano ya Shirikisho la Soka la Ulaya (Uefa).

Hiyo ndiyo hatua ya robo fainali, kwa maana kwamba zitachezwa mechi nne zitakazoamua timu nne zitakazokwenda nusu na kisha kubaki mbili zitakazoumana fainali.

Msimu huu, maji yalizidi unga kwa mabingwa watetezi, Real Madrid, ambao safari yao ilikwamia hatua ya 16 bora, wakiondoshwa na wababe wa soka la Uholanzi, Ajax.

Je, ubingwa wa mashindano hayo utatua wapi msimu huu? Ni England (Man City, Liverpool, Man United na Tottenham), Hispania (Barcelona), Italia (Juventus), Ureno (Porto) au Uholanzi (Ajax)?

Ajax

Ni kikosi kinachoundwa na asilimia kubwa ya wachezaji wenye umri mdogo, lakini bado kimeweza kuiteka Ulaya kwa soka lake la kuvutia.

Nyota Frenkie De Jong na Matthijs de Ligt, wamekuwa silaha ya Ajax si tu Ligi ya Mabingwa, bali hata Ligi Kuu ya Uholanzi, ambako timu hiyo inashika nafasi ya pili kwenye msimamo, ikiwa imeachwa pointi mbili tu na PSV.

Ajax si ngeni katika michuano ya Uefa kwani imewahi kushinda mara tatu mfululizo taji la European Cup ikiwa na nyota kama Johan Cruyff na Johan Neeskens, Clarence Seedorf, Edgar Davids na Patrick Kluivert.

Ajax ilijihakikishia nafasi katika hatua hii ya robo kwa kuwasukuma nje wakali wa La Liga, Madrid, kwa kichapo cha mabao 4-1 katika mchezo wa mwisho uliochezwa katika ardhi ya Hispania.

Barcelona

Ukweli ni kwamba, katika miaka saba iliyopita, Barca wamecheza fainali moja tu ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, hivyo huenda msimu huu, Lionel Messi na wenzake wamepania kumaliza mkosi huo.

Messi alikuwa na mchango mkubwa wakati kikosi hicho kikiing’oa Lyon katika hatua ya 16 bora, akizipasia mara mbili nyavu za Wafaransa hao katika mchezo wa mwisho uliomalizika kwa Barca kushinda mabao 5-1.

Msimu huu, Barca wako vizuri kwani si tu wamejichimbia kileleni mwa msimamo wa La Liga, pia hivi karibuni walitinga fainali ya Copa del Rey kwa kuwachapa wapinzani wao wakubwa katika historia ya soka la Hispania, Madrid.

Juventus

Lengo la kumsajili kwa mpunga mrefu staa wa Kireno, Cristiano Ronaldo, halikuwa jingine zaidi ya kuchukua taji hili la Ligi ya Mabingwa, ambalo wamelisubiri kwa kwa miaka 23 sasa.

Ronaldo ameonekana kuwaonesha kuwa hawakukosea kumpeleka mjini Turin kwani baada ya Juve kuchapwa mabao 2-0 katika mchezo wa kwanza, alipachika ‘hat trick’ kuing’oa Atletico Madrid.

Endapo Ronaldo atawapa ubingwa msimu huu, ataungana na Clarence Seedorf, ambaye anabaki kuwa mchezaji pekee aliyeshinda taji la michuano hii akiwa na timu tatu tofauti.

Wakati huo huo, isisahaulike kuwa mabeki wa Juve, Giorgio Chiellini na Leonardo Bonucci, wanataka kumaliza soka lao wakiwa na kumbukumbu ya kuwa washindi wa mashindano hayo.

Liverpool

Msimu uliopita, walicheza fainali na sasa wameshatinga robo fainali, wakiwatoa wakali wa soka la Ujerumani, Bayern Munich.

Baada ya matokeo ya kutofungana katika mtanange wa kwanza uliochezwa England, wengi waliona safari ya Liverpool ingeishia hapo lakini waliweza kushinda mabao 3-1 mjini Munich.

Ujio wa beki kisiki, Virgil van Dijk, aliyetua Liverpool mwaka jana kwa dau la Dola za Marekani milioni 99 umeweza kuijenga upya safu ya ulinzi ya kocha Jurgen Klopp, ambayo awali ilikuwa ‘nyanya’.

Jeuri nyingine ya ‘Majogoo’ hao wa Anfield inatokana na uwepo wa kipa wao wa kimataifa wa Brazil, Alisson Becker, ambaye amekuwa akiokoa hatari nyingi langoni mwake.

Wanaoweza kubashiri kuwa safari ya Liverpool itaishia hatua hii ya robo fainali wakumbuke kilichowakuta Man City msimu uliopita.

Man City

Wachambuzi wa soka la Ulaya wanaiona Man City kuwa kwenye nafasi nzuri ya kutwaa ubingwa msimu huu.

Hoja ya wachambuzi inajengwa na upana wa kikosi cha kocha wao, Pep Guardiola, ambaye tayari ameshalifungia kabatini taji la Kombe la Ligi.

Tishio kwa wapinzani wake katika hatua hii ni kitendo cha kuitoa Schalke ya Ujerumani kwa kichapo kizito cha jumla ya mabao 10-2.

Man United

Miaka 20 tangu alipowapa Man United taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa bao lake la dakika za majeruhi dhidi ya Bayern, Ole Gunnar Solskjaer, anataka kulibeba akiwa mkuu wa benchi la ufundi.

Bila shaka kitendo cha kupindua matokeo dhidi ya PSG baada ya kutandikwa mabao 2-0 katika mchezo wa kwanza, tena uliochezwa Old Trafford, ni ujumbe tosha kwa wapinzani wake wa sasa?

Kuondoka kwa Jose Mourinho kumeonekana ‘kuifufua’ Man United, ambayo tangu Solskjaer alipokalia kiti chake imepoteza mechi moja tu ya Ligi Kuu ya England, huku nyota waliokuwa hawapewi nafasi kama Paul Pogba wakiwa silaha muhimu kikosini.

Porto

Huenda kila timu ingependa kukutana na Porto lakini ukweli ni kwamba vijana hao wa kocha Sergio Conceicao si wa kubezwa hata kidogo.

Porto hawajavuka robo tangu mwaka 2004, walipokuwa chini ya kocha mwenye maneno mengi, Mourinho.

Hata hivyo, safari hii, inaweza kuwa zamu yao kuandika historia kwa kuwa si tu kikosi chao kimeundwa na nyota wenye vipaji kutoka Amerika Kusini, pia kina wazoefu wa michuano hii.

Wanaye mlinda mlango wa zamani wa Real Madrid, Iker Casillas (37) na aliyewahi kuwa beki wake pale  Santiago Bernabeu, Pepe (36), ambaye alitua Porto Januari, mwaka huu.

Pia, kama ilivyo kwa Liverpool yenye Sadio Mane na Mohamed Salah, safu ya ushambuliaji ya Porto nayo ina nyota tishio kutoka Afrika, Moussa Marega (Mali), mfungaji bora wao wa Ligi ya Mabingwa, akiwa ameshaweka kambani mara sita.

Tottenham

Ni mara ya pili kwa Tottenham kutinga robo katika historia ya Ligi ya Mabingwa licha ya ubahili wao katika soko la usajili. Chini ya kocha wao, Mauricio Pochettino, Tottenham wamekuwa kwenye kiwango kizuri katika miaka ya hivi karibuni.

Ikiwa na mshambuliaji wa kimataifa wa England, Harry Kane, nyota wa Denmark, Christian Eriksen, timu hiyo si ya kubezwa.

Tottenham kuing’oa Borussia Dortmund yenye kiwango bora msimu huu wa Bundesliga inaweza kuwa habari yenye kutia hofu kwa timu zote saba zilizobaki katika hatua hii ya robo fainali.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*