Solskjaer atabiri Martial kumfikia Ronaldo

 LONDON, England

KOCHA wa muda wa Manchester United, Ole Gunnar Solskjaer, amesema kwamba anavyoamini staa wake, Anthony Martial, anaweza kufikia kiwango cha nyota wa Juventus,  Cristiano Ronaldo.

Martial amekuwa katika ubora wa hali ya juu tangu Desemba mwaka jana wakati  Solskjaer alipochukua nafasi ya Jose Mourinho, ambapo straika huyo raia wa Ufaransa ameshafunga mabao 11 likiwamo alilofunga mwishoni mwa wiki katika mchezo ambao waliondoka na ushindi wa 3-0 dhidi ya Fulham.

Katika mchezo huo, nyota huyo mwenye umri wa miaka 23, alifunga bao kali dhidi ya Fulham ambapo ilishuhudiwa nahodha wa zamani wa Man United, Gary Neville, akimfananisha na Ronaldo kwa jitihada zake binafsi alizokuwa akizionesha wakati akiitumikia klabu hiyo ya Old Trafford.

Kutokana na hali hiyo, Solskjaer anakubaliana naye na akampa kibarua  Martial kumfikia mshindi huyo mara tano wa tuzo ya mchezaji bora wa dunia Ballon d’Or, Ronaldo.

“Tulikuwa tukishindwa kumaliza mchezo na tulikuwa tukicheza soka bovu, lakini  Cristiano alikuwa akifunga kama hivyo,” alisema Solskjaer.

“Na yeye Martial amefanya kitu kama hicho. Endapo anataka kufikia kiwango cha Cristiano, Anthony anafahamu anachopaswa kukifanya ana kipaji,” aliongeza kocha huyo wa muda.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*