Solskjaer akiiba kengele aweke pamba masikioni

NA AYOUB HINJO

NI kwenye matatizo pekee ndipo mwanadamu hufahamu nguvu na uwezo ulio ndani yake.

Usiyachukie wala usichukie kwanini wewe umepata tatizo, Mungu hajawahi kumpa mja mzigo asioweza kuubeba. Linapokuja tatizo, furahi, kwa maana wakati wako wa kuigundua nguvu iliyo ndani yako umewadia.

Mwandishi wa vitabu Mmarekani, Hellen Keller, akiwa na miezi 19 tu duniani, alipata ulemavu wa macho na masikio.

Hakuweza kuona wala kusikia chochote tena kwa miaka 87 aliyoishi duniani tangu Juni 27, 1880 alipozaliwa kule Alabama, Marekani. Ni kupitia tatizo hilo, leo dunia inamkumbuka Hellen kama mlemavu wa kwanza wa macho na masikio duniani kupata digrii ya sanaa.

Kwa ukaribu zaidi ifikirie Manchester United ile ya Sir Alex Ferguson kwa kipindi chote alichoifundisha timu hiyo.

Hakuna kingine zaidi ya kuitaja kama moja ya timu kubwa katika uso wa dunia hii, waliishi katika pepo yao kila walilolifanya liligeuka kuwa dhahabu.

Ukiziweka kando Real Madrid na Barcelona, wale Manchester United ilibaki kuwa moja ya timu za ndoto kwa wachezaji wengi katika kila kona ya ulimwengu.

Iwe America, Afrika, Ulaya na kwingineko ambako kunatengeneza mabara saba katika ulimwengu huu, hiyo ndiyo ilikuwa Manchester United.

Miaka sita tangu Ferguson apunge mkono wa kwaheri, kila kitu kinaonekana kubadilika kwa kasi kubwa ya ajabu pengine kuliko hata mbio za Hussein Bolt.

Imekuwa timu ya kawaida zaidi, kwa kifupi limebaki jina na historia yao ya kuvutia ambayo ilijengwa kwa miaka 26 ya kocha huyo mkongwe aliyeamua kukaa kando.

Tayari makocha wanne wamepita, yaani David Moyes, Ryan Giggs aliyefundisha kwa muda mfupi, akaja Louis van Gaal, kisha msema ovyo Jose Mourinho, wote hao walifunguliwa mlango wa kutokea.

Wote wanne waliishi kwa mashaka makubwa, kuanzia Carrington mpaka Old Trafford palikuwa pagumu kwao, tena cha kushangaza hakuna ambaye alibahatika kufundisha timu hiyo kwa miaka mitatu.

Pamoja na yote, kuanzia kwa Moyes mpaka Mourinho wote lawama zao wamezituma kwa uongozi ambao unaongozwa na Ed Woodward kwa kushindwa kutekeleza mahitaji yao.

Pengine kila mmoja atawaangalia katika sura ya usajili ambao walifanyiwa na mabosi hao, japo ni kundi kubwa la wachezaji wenye viwango vya kawaida walisajiliwa ndani ya Manchester United.

Kikubwa ambacho kinawaumiza wengi ndani ya kikosi hicho ni makocha kushindwa kuwa na kauli ya mwisho kwenye timu, uongozi ndio unaamua kila kitu.

Kingine kikubwa ambacho kinatoa hukumu kwa makocha wa Manchester United ni kile kizazi cha mwaka 1992, ndio mafanikio ya timu hiyo asilimia 70 yalikuwa katika miguu yao.

Ukifungulia Sky Sports unamwona Paul Scholes akiongea, ukiweka BT Sports utawaona akina Gary Neville wakikosoa, wamekuwa na midomo ambayo kwa kiasi fulani inaakisi kilichopo ndani ya timu yao pendwa.

Kwa kipindi chao chote hawakukutana na kadhia hiyo, wanaamini wachezaji wanaoingia United sasa hivi wanafuata pesa, inawezekana kwa upande mwingine.

Desemba mwaka jana, Manchester United walimtimua Mourinho na nafasi yake aliichukua Ole Gunnar Solskjaer, mchezaji wa zamani wa kikosi hicho.

Kama ilivyo kwa makocha wengine waliopita hivi karibuni, hata Solskjaer naye alikuwa na mwanzo mzuri, tena kuliko hata Ferguson.

Mambo yalionekana kumnyookea kama kumsukuma mlevi kwenye mtaro wa maji au mteremko mkali, vijana wa mitaa wanakwambia breki zimekata.

Lakini katika miezi miwili tangu apewe mkataba mambo yalibadilika, kila kilicho kizuri kilipotea, mabaya yalichukua nafasi, hakuna kinachoeleweka kwao.

Imekuwa kawaida Manchester United kuwa na malengo ya kumaliza ndani ya ‘top four’ tangu Ferguson alipoondoka na ubingwa wake wa mwisho wa Ligi Kuu.

Kwa jicho la tatu, tatizo la kawaida linaanzia juu kisha kushuka chini kwa wachezaji, yaani tuanzie kwa Woodward mpaka kwa akina Paul Pogba.

Solskjaer ataanza msimu ujao akiwa katika benchi hilo, tayari ameshapiga mkwara mzito wachezaji wake kujitunza katika likizo yao.

Hivi karibuni ameongea mambo mengi ambayo kama yakifanikiwa, basi historia itaandikwa, pengine hataki kuwa kama Liverpool ambao walikaa miaka mingi kama timu ya kawaida.

Kwa kila kinachoendelea ndani ya Manchester United, Solskjaer hana budi kusimama katika misingi aliyojiwekea japo hana sauti ya kuamua kila kitu kama ilivyokuwa kwa Ferguson.

Wala hana tofauti na mwizi wa kengele, ili aweze kukimbia au kuondoka nayo inabidi aweke pamba masikioni, asisikie jinsi inavyojigonga. Unajua kwanini?

Kwa ufupi tu, itamkatisha tamaa na anaweza akaitupa kwa kuhofia kukamatwa, Solskjaer ana kazi kubwa sana ndani ya Manchester United.

Aweke pamba masikioni kukwepa sauti za akina Scholes na Neville, ikiwezekana azime na macho kutosoma kila kinachoandikwa kuhusu timu yake mitandaoni au magazetini.

Kila mmoja anaisubiri Manchester United msimu ujao, dunia nzima inasubiri.  


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*