SINGIDA WALICHUKUA KOCHA NA MPIRA WA YANGA

NA ALLY KAMWE -

INAHITAJI uwe na macho ya kawaida kabisa. Elimu ya kawaida kabisa. Kichwa cha kawaida kabisa kuona ubora wa kikosi cha Singida United chini ya Hans van Pluijm.

Bahati mbaya sana hawana kundi kubwa la mashabiki mitaani na pengine ndio sababu ya kuwa mbali sana na kalamu za waandishi wa habari.

Hatuwaoni wakisifiwa katika kurasa za mbele za magazeti kama wengine lakini uwanjani Singida United ni timu tofauti kabisa. Ni timu inayovutia kuitazama kila dakika.

Soka lao linasisimua. Soka lao ni la hesabu kubwa.

Kwenye Kombe la Mapinduzi walituonyesha ladha ya mpira tuliyokosa katika timu kongwe za Kariakoo. Walipohitaji kutawala mchezo, ungeshuhudia pasi fupi fupi zikitembea kwa uhakika.

Walipohitaji bao, ungeona mipira mirefu na pasi za haraka zikitembea kutoka katikati ya uwanja kwa kina Deus Kaseke na Danny Lyanga.

Dhidi ya Azam, Singida walikosa matokeo tu. Na si kitu kipya kwenye soka, wanaofuatilia mpira wanaelewa. Huwa inatokea mara nyingi timu bora duniani kupoteza mchezo.

Kila shabiki aliridhika na uwezo wao. Hata baadhi ya viongozi na wachezaji wa Azam walikiri kupata tabu kucheza na Singida.

Unaweza kujiuliza nini kimeifanya Singida kuwa tishio kiasi hiki? Nini kilichoibadilisha Singida haraka hivi?

Jibu ni rahisi sana. Akili kubwa ya Hans van Pluijm iko kazini.

Ni Pluijm ndiye aliyeifanya Singida kuwa dude linaloogopesha katika soka la Tanzania hivi sasa. Ni Pluijm aliyewafanya hata Simba kukimbilia Morogoro kuweka kambi kujiandaa na mchezo dhidi yao.

Pluijm ni mwalimu wa mpira. Niliwahi kusema hili siku za nyuma na ninasema tena. Tanzania wamepita makocha wengi wakubwa, wenye CV za kutisha, lakini Hans van Pluijm ni kiboko.

Kichwa chake kina madini mengi ya soka. Ana uwezo wa kuibadilisha nyeusi kuwa nyeupe kwa muda mfupi na kwa ufasaha.

Jipe kazi rahisi tu. Ikumbuke Yanga ilivyokuwa chini yake kisha itazame Yanga hii chini ya George Lwandamina. Ni vitu viwili tofauti.

Sina maana kwamba Yanga ya Lwandamina ni mbovu, ni timu nzuri lakini Yanga ya Pluijm ilikuwa bora zaidi. Bora na tishio.

Kuanzia kwenye mifumo na mbinu za kutafuta matokeo, Pluijm aliifanya Yanga kuwa tishio ndani na nje ya mipaka ya Tanzania.

Sitaki kukumbusha sana kuhusu ufalme wa Yanga ya Pluijm kwenye soka la Tanzania, hilo linafahamika. Ninachotaka kukumbusha ni jinsi timu za Waarabu zilivyoanza kuwa na hofu na Yanga ya kipindi kile.

Ni Pluijm ndiye aliyewafanya kusubiri hadi dakika ya mwisho kuiondoa Yanga kwenye michuano ya Afrika. Ni Pluijm ndiye aliyeifanya Al Ahly kupotea katika ardhi yao.

Yanga ya Lwandamina inapata matokeo lakini kwa asilimia kubwa inategemea uwezo wa mchezaji mmoja mmoja na si muunganiko wa timu kwa ujumla.

Siku Ajib na Chirwa wakiamka vizuri, Yanga itashinda. Siku wakiamka vibaya, kila kitu kinakuwa kibaya. Usingeona hili kwa Pluijm.

Yanga bila fundi Haruna Niyonzima iliwatesa mno Etoile du Sahel. Yanga bila Donald Ngoma, iliwapeleka puta Mo Bejaia. Kama Chirwa angekuwa makini kipindi kile, hadithi ingekuwa tofauti kipindi hiki.

Hivi ndivyo Yanga ilivyotengenezwa kiufundi na Pluijm kisha ikabomolewa na Lwandamina. Yanga ya sasa imekuwa ikitegemea ubora wa mchezaji kupata matokeo na si uimara wa kikosi kwa ujumla.

Dhidi ya Azam, wangapi walikuwa wanajua kuwa Singida walicheza bila Mudathir Yahya? Hiki ndicho ninachokimaanisha kwa Pluijm. Timu yake huwa bora kwa mbinu na si uwezo wa mtu mmoja.

Mdogo wangu Mohammed Kamwe, mpaka leo haelewi ni taaluma gani waliyoitumia viongozi wa Yanga hadi wakachagua kubaki na Lwandamina na kumtema Pluijm.

Kama kuna kamari kubwa iliyowahi kuchezwa na Yanga katika kipindi cha miaka 10 ya hivi karibuni, basi uamuzi huu wa kumtega Pluijm unashika namba moja ukiacha ishu ya usajili wa Haruna Niyonzima.

Pluijm hahitaji sana kalamu yangu ili watu waelewe ubora wake. Anachokifanya na Singida United, msimu huu kinatosha kabisa kutufanya tumpe heshima yake.

Singida walinufaika sana na kamari iliyochezwa na viongozi wa Yanga.

Walimbeba kocha wao na mpira wao. Walichobakiza Yanga kwa sasa ni sifa magazetini tu lakini ile ‘kampa kampa tena’ iko Singida United. Ni chungu lakini tumeze ili tupone.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*