SIMEONE AMPONGEZA TORRES KUFIKISHA MABAO 100

 MADRID, Hispania   | 

KOCHA wa Atletico Madrid, Diego Simeone, amempongeza straika wake, Fernando Torres, akisema kwamba ni shujaa baada ya kufikisha mabao 100 katika michuano ya LaLiga wakati wa mchezo wa juzi ambao waliibuka na usindi wa mabao 3-0 dhidi ya Levante.

Staa huyo mwenye umri wa miaka 34, alitangaza mapema wiki iliyopita kwamba, ataondoka ndani ya klabu hiyo ambako alijitengenezea jina tangu akiwa mtoto wakati mkataba wake utakapomalizika mwishoni mwa msimu huu.

Torres ambaye alirejea Atletico mwaka 2015 awali kwa mkopo, anadaiwa kuwa alikuwa akisubiri kutimiza idadi hiyo ya mabao tangu Januari mwaka huu alipofunga la kwanza la LaLiga dhidi ya Las Palmas.

Hata hivyo, sasa ameweza kutimiza ndoto hiyo baada ya juzi kupachika bao hilo ambalo lilionekana kumkuna Simeone ambaye hakusita kummwagia sifa.

“Fernando ndiye shujaa mahali hapa, aidha awe amefunga ama asifunge,”     alisema kocha huyo katika mkutano na waandishi wa habari mara baada ya mechi hiyo.

“Anastahili sifa hiyo na ameshajijengea heshima kubwa kutokana na kazi anayoifanya. Wakati nilipomwita aje kusajiliwa na sisi, nimemweleza nataka awe mchezaji na wala si kuwa shabiki,”     aliongeza kocha huyo.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*