Simeone ampa tano Oblak

MADRID, Hispania

KOCHA Diego Simeone amempa tano mlinda mlango wake, Jan Oblak, akimwelezea kuwa ndiye bora duniani baada ya staa huyo kuiwezesha Atletico Madrid kupata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya  Celta Vigo katika michuano ya Ligi Kuu ya Hispania.

Katika mchezo huo wa juzi, Atletico waliweza kuzinduka katika kipigo cha wiki iliyopita cha mabao  2-0 kutoka kwa Barcelona na kufanikiwa kupata mabao hayo ambayo yaliwekwa kimiani na nyota wao, Antoine Griezmann na Alvaro Morata na hivyo wakaondoka na pointi zote tatu.

Hata hivyo, matokeo yangekuwa tofauti kama si umahiri wa  Oblak, ambaye aliokoa michomo mitatu ya hatari kutoka kwa nyota wa Celta Vigo.

Kufuatia kiwango hicho, Simeone anasema kwamba hana wasiwasi nyota huyo raia wa Slovenia ambaye alijiunga na klabu hiyo mwaka 2014 akitokea Benfica ndiye mlinda mlango bora kwa sasa katika nafasi hiyo.

“Ndiye mlinda mlango bora duniani,” alisema kocha huyo. “Tuna bahati sana kwake yeye kuamua kuichezea Atletico na ndiyo maana tuko naye,” aliongeza kocha huyo.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*