googleAds

SIMBU, MAGDALENA WAKIWEZESHWA MAPEMA TANZANIA ITANG’ARA LONDON

NA HASSAN DAUDI

FILBERT Bayi ni miongoni mwa wanariadha wachache waliowahi kuipeperusha vema bendera ya Tanzania katika michuano ya kimataifa.

Mwaka 1973 akawa mshindi wa mbio za mita 1500 katika michuano ya All-Africa Games kabla ya kutetea ubingwa wake miaka mitano baadaye.

Bayi mzaliwa wa Arusha, alitwaa medali ya dhahabu katika michuano ya Jumuiya ya Madola na hiyo ilikuwa mwaka 1974 nchini New Zealand.

Aliyeshika nafasi ya pili ni John Walker wa New Zealand na Mkenya Ben Jipcho.

Katikla michuano ya Olimpiki ya mwaka 1980 iliyofanyika jijini Moscow, Urusi, Bayi aliibeba tena na baada ya kushinda medali ya shaba katika mbio za mita 3000.

Mpaka leo Bayi anatajwa kuwa mmoja kati ya wanariadha wakubwa wa mbio za mita 1500.

Wengine ambao majina yao yamebaki kwenye historia ya mchezo huo hapa nchini kutokana na kile walichokifanya kwenye mashindano ya kimataifa, ni Juma Ikangaa na Suleiman Nyambui.

Ni miaka mingi imepita tangu Tanzania ilipokuwa ikifua dafu kwenye mashindano ya kimataifa ya mchezo wa riadha.

Mara baada ya kuondoka kwa wakongwe hao, Bayi, Ikangaa na Nyambui, ni kama mchezo wa riadha umekufa.

Wanariadha wengi wanaokwenda kuiwakilisha Tanzania kwenye michuano ya kimataifa wamekuwa wakiambulia patupu.

Wapo wanaoamini kuwa moja kati ya sababu kubwa ambayo imekuwa ikitajwa kuchangia ‘kifo cha mende’ kwa wanariadha wetu kwenye mashindano ya nje ya nchi ni maandalizi ya zima moto.

Bila shaka sasa Tanzania inajivunia ubora alionao mwanariadha Alphonce Simbu, ambaye aling’ara kwenye mbio za Standard Chartered Mumbai Marathon zilizofanyika hivi karibuni nchini India.

Simbu alitumia saa 2:09:32 kuibuka kidedea kwenye mbio hizo na aliyeshika nafasi ya pili, Mhindi Bahadur Singh Dhoni alitumia saa 2:19:51.

Baada ya kuwa mshindi katika michuano hiyo, Simbu ataiwakilisha Tanzania kwenye mashindano ya riadha ya dunia.

Itakumbukwa pia kuwa Simbu aliipeperusha vema bendera ya Tanzania katika michuano ya Olimpiki iliyofanyika jijini Rio, Brazil, ambapo alishika nafasi ya tano.

Bila shaka nyota huyo anastahili pongezi kubwa kwa mchango wake katika kuupigania mchezo wa riadha ngazi ya kimataifa.

Mbali na Simbu, mwanadada Magdalena Crispian, alikuwa mwakilishi mwingine wa Tanzania ambaye alifanya vizuri nchini India.

Magdalena ambaye alitumia saa 2:34:51 kumaliza mbio za kilomita 31, alishika nafasi ya nne kwa upande wa wanawake.

Kwa matokeo hayo, Tanzania itakuwa na wawakilishi wawili katika mbio za dunia za mwaka huu.

Naamini kuwa ili Tanzania iweze kufanya vizuri katika michuano hiyo ya kimataifa, mipango madhubuti ya kuwawezesha Simbu na Magdalena kuwika kwenye mashindano hayo yatakayoanza kutimua vumbi Agosti mwaka huu jijini London, Uingereza, inatakiwa kuanza sasa.

Kwa tathmini ya haraka, ni kipindi kisichozidi miezi saba kimebaki kabla ya kuanza kwa michuano hiyo ya jijini London.

Naamini kuwa ni kipindi kirefu ikiwa Shirikisho la Riadha (RT) kwa kushirikiana na Serikali, litakitumia vizuri kuwaandaa mashujaa hao.

Kwa kuzingatia ugumu wa mashindano hayo ambayo yatawakilisha nchi nyingi na zilizopiga hatua katika mchezo wa riadha, natamani kuona mastaa hao wakiingia kambini mapema.

Simbu na Magdalena wanapaswa kuandaliwa mazingira yatakayowawezesha kufanya vizuri pale London la sivyo watakwenda kusindikiza tu.

Kama watapewa maandalizi ya kukurupuka, basi haitashangaza hata kidogo kuwaona mastaa hao wakirejea nchini vichwa chini kama ambavyo tumekuwa tukipokea wawakilishi wengine pale Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere.

Tukiri kuwa wanariadha hao wamepambana vya kutosha kufika hapo walipo leo hii.

Ndiyo, hakuna mipango yoyote ya kueleweka katika kuinua mchezo wa riadha hapa nchini. Hakuna ‘academy’, na hata miundombinu ya riadha ni kichefuchefu tu.

Hakuna ubishi kuwa hata hao waliofanikiwa katika mchezo huo, wakiwamo Bayi, Ikangaa na Nyambui walitumia nguvu ya ziada kuipeperusha bendera ya Tanzania katika michuano ya kimataifa.

Ili kuwa na uhakika wa kuwaona Simbu na Magdalena wakifanya vema jijini London, lazima kuwapo kwa mipango ya mapema na si kutegemea bahati.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*