Simba, Yanga mwendelezo wa vituko kujitoa Kagame

NA HASSAN DAUDI

NILIANZA kusikia Simba haitakuwa sehemu ya michuano ya Klabu Bingwa Afrika na Kati, maarufu Kombe la  Kagame.

Wakati nikifikiria uzito wa sababu walizozitoa, ghafla Yanga nao wakafuata nyayo.

Michuano  hiyo  inayoandaliwa na  CECAFA (Baraza la Vyama Vya Soka Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati) inatarajiwa kuanza Julai, mwaka huu, nchini Rwanda.

Kama walivyofanya wenzao hao wa Kariakoo, nao wakatangaza kutoshiriki michuano hiyo, huku sababu ya uamuzi wao ikikosa mantiki.

Nikirejea kwa Wekundu wa Msimbazi, mabingwa wa Ligi Kuu msimu uliokwisha, kwa mtazamo wangu, ambao si rahisi kufafana na kila mmoja, sikuona uzito wa sababu zao.

Kwamba wanajiweka kando ya Kombe la Kagame kwa kuwa wanajiandaa na msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara na mashindano ya kimataifa.

Wakati nikijaribu kutafuta mantiki ya kile walichodai, sababu ya Yanga ikanivuruga zaidi. Eti hawana kikosi kwa kuwa sehemu kubwa ya wachezaji wake wamemaliza mikataba.

Tuanze tafakuri yetu kwa kila moja, tukitupa karata ya kwanza kwa Wekundu wa Msimbazi.

Nini kilichowafanya waliochukua uamuzi kujiridhisha kuwa Kombe la Kagame si sehemu sahihi ya maandalizi?

Je, ni michuano gani mingine ya hadhi hiyo iliyoko mbele yao wanayoamini ndiyo itakayowasaidi kujiweka fiti kuelekea msimu ujao?

Huenda jibu la haraka litakuwa ni mechi watakazotafuta kujiandaa na msimu ujao ‘pre-season’, ambazo ukweli ni kwamba haziwezi kufikia ushindani wa Kombe la Kagame.

Mwishowe, ni mwendelezo wa kuoneshana mbwembwe za kambi katika mataifa ya Ulaya, huku zikiwa na tija ndogo linapokuja suala la kuimarisha kiwango cha kikosi.

Tukija kwa upande wa Yanga, sababu yao ilikuwa kituko na aibu kubwa hata mbele ya kila shabiki wa timu hiyo ya Jangwani. Timu haitakwenda Rwanda kwa kuwa haina kikosi kamili!

Ni kweli kocha wao raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) atakuwa Misri zitakakofanyika fainali za Afcon 2019,  lakini bado hiyo haitoshi kuiondoa Yanga katika mashindano hayo.

Wengi watakumbuka kuwa katika baadhi ya mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara msimu uliopita, Yanga walishuka dimbani bila huduma ya mkufunzi huyo? Kwanini leo hii hilo lionekane geni kwa Kombe la Kagame?

Tukija kwa wachezaji sasa, lazima ukweli uwe hivi, wengi wao wamemaliza mikataba yao. Ni kama walivyosema wenyewe Yanga, hawana kikosi kamili.

Hapo swali ni je, ni katika ulimwengu upi wa soka tunamoishi? Mbona kila siku tunapishana na kinachoendelea duniani? Hivi, wapi kwingine unakoweza kulikuta hilo la msimu ukiisha, huku asilimia kubwa ya wachezaji wakiwa si mali ya klabu?

Kwa kile ninachokitambua, kutokana na uzoefu wangu wa masuala ya soka, ukichangiwa zaidi na kile ambacho tumekuwa tukikishuhudia katika mataifa yaliyo ‘serious’, huwezi kukutana na aibu ya aina hii.

Nitakutolea mfano mdogo katika hilo. Ibrahim Ajib ni mchezaji tegemeo katika kikosi cha Yanga, ikifikia hatua ya kukabidhiwa kitambaa cha unahodha. Cha kushangaza, ni sehemu waliomaliza mikataba yao.

Ni kwa maana kwamba, ikiwa Ajib ataondoka Jangwani, viongozi wa Yanga wanatakiwa kuwajibishwa na wanachama na mashabiki wa klabu hiyo, mabingwa wa kihistoria Ligi Kuu Bara.

Kwanini nasema hivyo, ni kwa kuwa suala la kumpiga kitanzi lilitakiwa kushughulikiwa mapema na si kama ilivyo sasa ambapo mashabiki wa Yanga hawana raha kutokana na tetesi zinazoendelea kuwa amesaini mktaba wa awali Msimbazi.

Katika hilo la uzembe wa viongozi kukabiliana na presha ya kuwapoteza wachezaji tegemeo, ningeweza kumtaja pia Papy Tshishimbi, ambaye almanusura akimbie, kabla ya kupewa mkataba mpya akiwa mchezaji huru.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*