SIMBA YAMALIZA TATIZO

NA ZAITUNI KIBWANA

AMETUA mwanangu! Yule kipa mwenye rekodi ya kutwaa Taji la Dunia, ametua nchini jana tayari kuwatumikia Wekundu wa Msimbazi, Simba kwenye michuano ya Ligi Kuu Tanzania Bara.

Kipa huyo, Daniel Agyei (27), kutoka Ghana pia alikuwa kikwazo kikubwa kwa Yanga kupata ushindi kwenye mechi mbili za robo fainali ya Kombe la Shirikisho wakati akiwa langoni kuilinda Madeama.

Agyei ametua jana kwenye Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Julius Nyerere (JNIA) saa 7:30 mchana, ameletwa kwenye kikosi cha Simba kwa ajili ya kuongeza nguvu hasa katika kulinda lango la timu hiyo.

Kipa huyo aliyecheza timu mbalimbali kama Free State Stars, Liberty Professionals na Medeama, anashikilia rekodi ya dunia kwa kutwaa ubingwa wa Kombe la Dunia la Vijana chini ya miaka 20, ambapo kipa huyu alikuwa shujaa wa Ghana baada ya kuokoa penalti mbili katika ushindi wa penalti 4-3 dhidi ya Brazil.

Kwa rekodi hiyo, Simba inakuwa timu ya kwanza Tanzania kupata mchezaji aliyewahi kuchukua Kombe la Dunia, ambapo pia alitwaa Kombe la Mataifa ya Afrika la Vijana chini ya miaka 20 mwaka 2009.

Agyei pia alikuwa kwenye kikosi cha Ghana kilichoshika nafasi ya pili katika Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka 2010 nchini Angola, ambapo alikuwa kipa namba mbili kwenye kikosi cha Ghana, licha ya kwamba hakucheza mechi hata moja kutokana na uwepo wa kipa mahiri, Richard Kingson.

Akizungumza mara baada ya kuwasili na kupekelewa na Meneja wa zamani wa timu hiyo, Abasi Ali, Agyei alisema amekuja kwa ajili ya kuleta changamoto mpya ndani ya Simba na kwenye soka la Tanzania.

“Nimekuja kuleta changamoto mpya, najua kuna makipa wapo kama Angban, namfahamu hivyo natambua kilichonileta ni kwa ajili ya kukubaliana na kila kitu,” alisema.

Alipoulizwa kuhusu Simba ambao kwa sasa ndio vinara wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Agyei alisema anatambua ukubwa wa timu hiyo ndiyo sababu iliyomfanya kutua nchini.

“Najua Simba ni timu kubwa ndio maana nipo hapa leo hii, ila ninachotaka kusema ni kwamba mchezaji maisha yake ni popote pale na mimi nimekuja kufanya kazi,” alisema.

Alipoulizwa kuhusu dau la Dola za Marekani 30,000 ambazo ni zaidi ya Sh milioni 65 alizozitaka kwenye usajili wake, Agyei hakutaka kuzungumzia na kusema kuwa mpaka akae na viongozi wa Simba ndio atakuwa na nafasi nzuri ya kulisemea hilo.

Agyei ambaye ndiye kipa chaguo la kwanza la timu ya taifa ya Ghana, alikuja kwa mara ya kwanza nchini kuivaa Yanga katika mechi ya Kundi A ya mashindano ya Kombe la Shirikisho.

Simba imelazimika kutafuta kipa mwingine wa kusaidiana na Angban kutokana na kipa huyo kukosa msaidizi hasa baada ya Manyika Peter kushindwa kutoa changamoto. Lakini pia ni kutokana na kiwango cha Angban kuwa cha wasiwasi katika baadhi ya mechi.

Wekundu hao wa Msimbazi katika mzunguko wa kwanza, walikuwa wakimtegemea zaidi Angban aliyefungwa mabao sita na kuwaacha wenzake benchi kama Peter Manyika na Denis Richard ambao hawajapata nafasi kwenye kikosi hicho.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*