SIMBA YAIZIDI UJANJA YANGA KWA BOSSOU

EZEKIEL TENDWA NA SAADA SALIM


SIMBA wajanja sana aisee. Kumbe wakati Kocha Mkuu wa kikosi hicho, Joseph Omog, alivyokuwa akimuweka benchi beki wao kisiki, Jjuuko Murushid, alikuwa na maana yake kubwa, huku Yanga wao wakiendelea kumtumia Vincent Bossou bila kujua nini kitakuja mbele yao.

Unajua ikoje! Simba watamkosa Murushid kwa kipindi cha Januari, ndiyo maana wakaamua kumuweka benchi baadhi ya michezo yao ili Novaty Lufunga azoeane na Method Mwanjali, lakini Yanga wao hawakushtuka wakaendelea kumtumia Bossou.

Yanga walishindwa kushtuka kwamba watamkosa Bossou, ambaye ataiwakilisha nchi yake ya Togo kwenye michuano ya AFCON, wakaendelea kumpa nafasi kubwa ya kucheza, tofauti na Simba, walioshtuka mapema wakamuweka benchi Murushid, ambaye naye atakuwa na timu yake ya Uganda ‘The Crane’ huko AFCON.

Hiyo ina maana kuwa, Kocha Mkuu wa Yanga, George Lwandamina, atakuwa na kibarua kigumu cha kumtengeneza Kelvin Yondani ili aendane sawa na Andrew Vincent ‘Dante’, ambao ndio watakuwa na jukumu la kuilinda ngome yao.

Kama mmojawapo kati ya hao atakuwa na kiwango cha chini au atapata majeraha ni wazi nahodha Nadir Haroub ‘Cannavaro’ ambaye muda mwingi amekuwa akisugulishwa benchi, itabidi apangwe ili kuokoa jahazi.

Mbali ya Cannavaro, pia ikibidi sana wanaweza wakamchezesha Mbuyu Twitte nafasi hiyo, licha ya kwamba zipo taarifa kuwa itabidi ajitume sana, kwani ni kati ya wachezaji wanaotajwa kwamba wanaweza kupitiwa na panga la Lwandamina.

Kukosekana kwa Bossou, ambaye amekuwa tegemeo katika kikosi hicho, kunatajwa kuwa kunaweza kukaleta athari, hasa wakati huu ambapo wanapigania kutetea ubingwa wao mbele ya watani zao, Simba, ambao msimu huu wanaonekana kushika kasi.

Kwa upande wao Simba, hata hawana presha na kukosekana kwa Murushid katika baadhi ya michezo hiyo, kwani Lufunga na Mwanjali wameshatengeneza kombinesheni ya hatari na ukuta wao haupitiki kirahisi.

Awali wakati Omog akimpa nafasi Lufunga na kumuweka benchi Murushid, baadhi ya mashabiki walikuwa wakilalamika, kumbe kocha huyo alikuwa na maana yake kubwa kwamba itafika wakati atamkosa Mganda huyo.

Omog aliwahi kuliambia BINGWA kuwa, analazimika kumtumia Lufunga na Mwanjali, kwani anajua kwamba atamkosa Murushid Januari, hivyo lazima aanze kutengeneza ukuta wake kwa kuwatumia wawili hao ambao wao watakuwepo tu.

Majibu hayo ya Omog yalitokana na malalamiko ya baadhi ya mashabiki waliokuwa wakihoji kitendo cha kumuweka benchi Murushid, mwenye uwezo mkubwa na kumuanzisha Lufunga.

Wakati Omog akipiga mahesabu hayo, kwa upande wake, kocha wa zamani wa Yanga, ambaye kwa sasa ni mkurugenzi wa ufundi, Hans van der Pluijm, aliendelea kumpa nafasi kubwa Bossou, bila kujali kuwa atamkosa Januari.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*