SIMBA YAIFUATA NDANDA KIJESHI

ZAITUNI KIBWANA NA MWAMVITA MTANDA


 

KIKOSI cha Simba kinaondoka leo kuelekea Mtwara kwa ajili ya maandalizi ya mechi yao dhidi ya Ndanda FC, inayotarajiwa kuchezwa Jumamosi kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona, mkoani humo.

Akizungumza na BINGWA jana, Ofisa Habari wa Simba, Haji Manara, alisema kikosi kipo kamili na wamejiandaa  ipasavyo kukabiliana na mechi hiyo, pia kinatarajia kuondoka saa 5:00 na Ndege ya Shirika la Precision.

“Kikosi kipo kamili na hakuna majeruhi, tunatarajia kuondoka mapema saa tano asubuhi, lengo tuwahi kufika na wachezaji wapate muda wa kupumzika, wawe fiti kwa ajili ya kupambana,” alisema Manara.

Manara alisema ana uhakika na kikosi chao kuibuka na ushindi katika mechi hiyo, kutokana na maandalizi mazito waliyopata kutoka kwa kocha wao, Patrick Aussems.

“Sijawahi kuwa na mashaka juu ya kikosi cha Simba kwa timu yoyote ambayo watakutana nayo, kwanza wachezaji wake wanajiamini na hata kocha wao yupo vizuri na imani kwa asilimia kubwa tutawafunga Ndanda na tutarudi nyumbani na ushindi,” alisema Manara.

Hii ni mechi ya tatu tangu kuanza kwa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu, ambapo mechi yao ya kwanza walivaana na Prisons na kushinda bao 1-0, kabla ya kuichapa Mbeya City mabao 2-0.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*