SIMBA YAHUSISHWA KUVURUNDA KWA AZAM

NA WINFRIDA MTOI    |   

NAHODHA wa kikosi cha Azam FC, Himidi Mao, amekiri kuwa nafasi waliyopo kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, inawachanganya wachezaji na kuwafanya wavurunde katika mechi zao.

Tofauti ya pointi kati ya Wanalambalamba hao na vinara wa ligi Simba, imeonekana dhahiri kuwavuruga Azam, ambayo ipo nafasi ya tatu katika msimamo wa ligi hiyo, ikiwa na pointi 46 baada ya kucheza mechi 24, huku Simba ikiongoza na pointi 55 kabla ya mechi ya jana na Yanga nafasi ya pili na pointi 47, ikicheza michezo 22.

Akizungumza baada ya mchezo wao dhidi ya Njombe Mji juzi, Himid alisema wanachopitia ni kitu kipya kwao kwa sababu mara nyingi inapofikia kipindi kama hiki, wanakuwa kileleni au kupishana kwa pointi chache na anayeongoza.

Alisema kutokana na mazoea hayo, kitendo cha kuachwa pointi nyingi na timu iliyopo juu, kinawasumbua akili wachezaji na kuwafanya wacheze mechi kwa presha kutafuta ushindi huku timu nyingi zikiwakamia.

“Kinachoitokea timu yetu msimu huu ni kitu kipya, hatujakizoea kwa sababu katika misimu mingi iliyopita, ikifika kipindi hiki tunakimbizana katika nafasi mbili za juu katika msimamo wa ligi, lakini hali imekuwa tofauti na inatuchanganya,” alisema.

Katika hatua nyingine, kocha mkuu wa timu hiyo, huenda akakumbana na rungu la adhabu ya Shirikisho la Soka Tanzania, baada ya juzi kutolewa nje na mwamuzi aliyechezesha mechi yao na Njombe, Jonesia Rukyaa.

Kocha huyo ambaye aliwahi kupewa adhabu kama hiyo mara mbili msimu huu, alitolewa dakika tano kabla ya mchezo huo kumalizika na kwenda kukaa jukwaani.

Kutokana na hilo, atakuwa nje wakati timu yake itakapovaana na Mtibwa Sugar, mwishoni mwa wiki hii, Manungu, Morogoro.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*