googleAds

Simba yageukia wabishi

WINFRIDA MTOI

SIMBA imeiweka kiporo UD Songo ya Msumbiji na badala yake, kuelekeza nguvu zao kwa Azam watakayocheza nayo katika mchezo wa Ngao ya Jamii, utakaopigwa Jumamosi kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Jumamosi iliyopita, Simba ilishuka dimbani ugenini kuvaana na UD Songo katika mchezo wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Afrika na kupata suluhu, matokeo yanayowapa nafasi kubwa ya kusonga mbele kuelekea mchezo wa marudiano kati ya Agosti 23 na 25, jijini Dar es Salaam.

Lakini kwa kufahamu azma yao ya kutoacha taji lolote msimu ujao, Simba imeamua kusahau habari za Ligi ya Mabingwa kwa muda na kuelekeza nguvu za Ngao ya Jamii.

Ikumbukwe kuwa Simba ndio wanaoshikilia ngao hiyo waliyoitwaa msimu uliopita kwa kuichapa Mtibwa Sugar mabao 2-0 kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.

Kuonyesha jinsi walivyoipania Azam, saa chache baada ya kikosi cha Simba kutua nchini kikitokea Msumbiji, alfajiri yake kilipelekwa mazoezini kwenye viwanja vya Gymkhana, kuendelea kunoa makali.

Na leo Wekundu wa Msimbazi hao wataendelea na mazoezi kwenye viwanja hivyo baada ya wachezaji kupewa mapumziko ya Sikukuu ya Idi iliyoadhimishwa jana.

Pamoja na kutamba kufanya usajili ‘bab kubwa’, Simba wanafahamu kuwa mchezo wao wa Jumamosi hautakuwa rahisi kwao kutokana na ukweli kuwa Azam huwa ni ‘wabishi’ mno wanapocheza na timu kongwe hapa nchini, Yanga na Wekundu wa Msimbazi hao.

Mchezo dhidi ya Azam, utakuwa ni nafasi ya pekee kwa wachezaji wapya wa Simba, kufahamu aina ya timu wanazotarajiwa kukutana nazo Ligi Kuu Tanzania Bara.

Wachezaji kama Msudan Sharaf Shiboub, Wabrazil Tairone Santos da Silva, Gerson Fraga Viera na Wilker Henrique da Silva, hawajawahi kucheza na timu za Tanzania, hivyo mchezo dhidi ya Azam utakuwa wa kwanza kwao.

Kwa upande wa Deo Kanda, aliwahi kukutana na Simba na Yanga wakati akiwa TP Mazembe, lakini katika michuano ya kimataifa kama ilivyo kwa Francis Kahata aliyetokea Gor Mahia ya Kenya.

Meneja wa Simba, Patrick Rweyemamu, aliliambia BINGWA kuwa wachezaji wote watarejea kambini leo na jioni saa 9:00 watakafanya mazoezi kujiandaa na mechi hiyo dhidi ya Azam.

“Tulitoa siku moja ya mapumziko kwa ajili ya Sikukuu, kesho (leo), mazoezi yanaanza rasmi, kujiandaa na mechi zetu, ikiwamo ya Ngao ya Jamii dhidi ya Azam FC,” alisema.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*